*********************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Mabingwa watetezi wa kombe la UMISSETA katika mchezo wa mpira wa wavu (Volleyball) timu ya wasichana ya Mtwara watakutana na timu ngumu ya Dar es salaam kesho katika mchezo wa kusisimua utakaochezwa katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.
Mtwara imeingia hatua hiyo baada ya kuichapa Mbeya seti 3-0 na Dar es salaam imefanikiwa kufika fainali baada ya kuitoa Mara kwa seti 3-0.
Mara baada ya mchezo huo kocha wa Mtwara Gabriel Joshua aliwapongeza wapinzani wake Mbeya kwa ushindani waliouonyesha katika mchezo huo ambapo katika seti ya tatu wenyeji Mtwara walilazimika kushinda seti hiyo kwa point 25-21.
Joshua alisema tangu kuanza kwa mashindano ya mwaka huu hakuna timu iliyoweza kupata pointi 15 hivyo amesifu kiwango cha Mbeya na mashindano ya mwaka huu kwa ujumla kwani timu pinzani zilionyesha kiwango cha uchezaji tofauti na miaka ya nyuma.
Akizungumzia mchezo wa fainali dhidi ya Dar es salaam, nahodha msaidizi wa Mtwara Proscovia Conrad alitamba kuwa timu yake itaigalagaza Dar es salaam na wala hatarajii kupata upinzani kutoka Dar es salaam kama alioupata kutoka kwa timu ya Mbeya.
Michezo ya nusu fainali ya wavulana ya mpira wa wavu itachezwa mchana huu katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.
Matokeo ya michezo mingine ya nusu fainali ya mpira wa mikono wasichana kati ya Unguja dhidi ya Morogoro, ambapo Unguja ilifungwa magoli 16-20, huku Geita dhidi ya Songwe 19-28.
Matokeo hayo yanaipa nafasi Morogoro kucheza na Dar es saaam hapo kesho katika fainali huku Geita na Unguja watacheza kutafuta mshindi wa tatu.
Kwa upande wa mpira wa kikapu timu zilizofuzu hatua ya nusu fainali ni Dar es salaam, Mwanza, Unguja na Morogoro kwa wasichana na wavulana ni Dar es salaam, Mwanza, Unguja na Morogoro.
Michezo yote ya nusu fainali itakamilika leo jioni na mechi za fainali zitachezwa kesho katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara isipokuwa mchezo wa fainali wa soka utachezwa keshokutwa katika uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara.