***************
Jumla ya vijana 4,000 wa mikoa ya Dodoma, Lindi na Manyara wanatarajia kunufaika na mafunzo maalum ya ufundi stadi yatakayowapa ujuzi na utayari wa kuajiriwa au kujiajiri, kupitia mradi wa Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo ya Tanzania, kwa kiingereza “Employment and Skills for Development Tanzania”.
Makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo yametiwa saini tarehe 28 Juni 2021, jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA) nchini Tanzania, Kyucheol Eo.
Akizungumza wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini Tanzania, Kyucheol Eo, amesema kuwa Serikali yake imetenga kiasi cha Dola za Kimarekani 5,300,000 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba utatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia 2021 hadi 2023.
Amesema VETA itashirikiana kwa karibu na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha vijana wa kitanzania wananufaika na ukuaji wa uchumi katika sekta zinazotegemea ujuzi wa ufundi stadi.
“KOICA inafurahi kushirikiana na VETA kusaidia vijana nchini Tanzania kupata ajira ikiwa ni pamoja na kujiajiri ili waweze kutimiza ndoto zao. Tutashirikiana pia na GIZ kutekeleza mradi huu ambao utanufaisha moja kwa moja vijana 4,000, ambapo kati yao 1,400 ni wanawake,” amesema Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini Tanzania, Kyucheol Eo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, ameishukuru Serikali ya Korea kwa ufadhili huo na kusema kuwa mradi huo umejikita katika kutoa mafunzo ya muda mfupi kwenye fani za Uchomeleaji (Welding), Ufundi Bomba wa Viwandani (Industrial Plumbing) na Mekatroniki (Mechatronics).
Amesema mradi huo, pamoja na mambo mengine, utawapatia vijana hao mafunzo ya ujasiriamali na kutoa fedha kama mtaji ili kuwawezesha wahitimu kuanzisha miradi yao na kuwawezesha kujiajiri. Mitaji hiyo itatolewa kwa timu za wanafunzi zitakazoshinda kupitia uwasilishaji wa miradi bora itakayopatikana kupitia shindano maalum la ujasiriamali litakalofanyika kila mwaka.
“Tuko tayari kutoa mafunzo kwa vijana hao 4,000 waliolengwa na mradi huu ambao tunaamini kuwa wakihitimu watakuwa na ujuzi utakaowawezesha kujipatia ajira na hasa kwa kuzingatia uwepo wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa nchini inayotoa fursa za ajira kwa vijana wengi wenye ujuzi,” Dkt. Bujulu amefafanua zaidi.
Katika mradi huo, KOICA pia itawezesha utoaji mafunzo kwa walimu wa ufundi stadi kwenye fani zitakazohusika, kufanya mapitio ya mitaala iliyopo na kutengeneza mipya pamoja na ununuzi wa mitambo na vifaa vya mafunzo.