Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt Philip Isdor Mpango akizungumza na Washiriki wa mkutano mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA)wa mwaka 2021,wakati akifungua mkutano huo uliofanyika Jijini Tanga.
Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA)wa mwaka 2021 wakimsikiliza mgeni Rasmi katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA)wa mwaka 2021, ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango. Mkutano huo Unafanyika Jijini Tanga.
Mufti Mkuu wa Tanzania , Sheikh Aboubakar Zuber Bin Ali akizungumza na washiriki wa mkutano mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA)wa mwaka 2021, wakati akimkaribisha mgeni Rasmi katika ufunguzi huo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango.
PICHA – OFISI YA MAKAMU WA RAIS
…………………………………………………………………………..
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP ISDOR MPANGO,
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO
MKUU WA BAKWATA
TAREHE 27 JUNI, 2021
REGAL NAIVERA HOTEL – TANGA
Mheshimiwa Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania;
Mheshimiwa Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Tanga;
Sheikh Khamis Said Mataka, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA Taifa;
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Ulamaa;
Mheshimiwa Mwalimu Nuhu Jabir Mruma, Katibu Mkuu BAKWATA;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya BAKWATA;
Waheshimiwa Masheikh wote na Viongozi wa BAKWATA mliopo;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini na Madhehebu Mbalimbali;
Viongozi wenzangu wa Chama na Serikali;
Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Wageni waalikwa, Waandishi wa Habari; Mabibi na Mabwana;
Assalaam Eleykum!
Napenda nianze, kwa kuungana na wote walionitangulia, kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukusanyika hapa siku hii ya leo tukiwa wenye afya njema. Aidha, nichukue fursa hii kumshukuru sana Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Ally Mbwana pamoja na uongozi mzima wa BAKWATA kwa kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mgeni rasmi katika Mkutano huu muhimu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA). Hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki nanyi katika Mkutano kama huu. Hivyo, kwangu mimi ni faraja kubwa sana kuwa sehemu ya washiriki wa Mkutano huu. Niwashukuru pia wajumbe wote ambao mmepata nafasi ya kuja, pamoja na kwamba wengine mnatoka mbali, lakini mmeweza kufika.
Kabla ya kuendelea, napenda kuwasilisha kwenu salam za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan kwako Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, na wajumbe wote wa Mkutano Mkuu. Mheshimiwa Rais anawasalimia na anawatakia Mkutano mwema na wenye mafanikio.
Mheshimiwa Mufti,
Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Moja ya majukumu ya viongozi wa dini ni kuwaelekeza waumini kiroho, na kijamii na hasa kuwahimiza wamche Mola wao. Hivyo, pamoja na huduma za kuwaelimisha wananchi kiroho, zipo pia huduma mbalimbali ambazo zinatolewa na taasisi zetu za kidini kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu. Naomba nitambue mchango mkubwa unaotolewa na BAKWATA katika shughuli mbalimbali za kijamii katika nchi yetu, mijini na hata vijijini. Ninafahamu kuwa, mnayo miradi mingi ya kijamii mnayoisimamia, hususan kwenye sekta ya: afya (vituo vya afya 18, zahanati 96); elimu (shule za awali 15, msingi 32, sekondari 175, kidato cha tano na sita 35, vyuo vya kati 4, vyuo vya ufundi 6, chuo kikuu 1), maji (visima zaidi ya 1,000) pamoja na vituo vya kutunzia Watoto yatima na wale wanaotoka kwenye mazingira magumu. Watanzania wengi wamenufaika na wanaendelea kunufaika na huduma za kijamii zinazotolewa na BAKWATA.
Serikali inawashukuru sana kwa mchango wenu huo mkubwa na tunawaomba muendelee kuwahudumia Watanzania, hasa wa kipato cha chini bila ubaguzi. Naomba kuwahakikishia kuwa Serikali inathamini sana mchango unaotolewa na BAKWATA katika jamii. Hakika BAKWATA imeendelea kuwa mdau muhimu na mshirika mzuri wa Serikali katika kuhudumia wananchi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1968. Ipo mifano mingi tu ambapo unakuta huduma za jamii nilizozitaja, zipo mahali ambapo hata Serikali bado haijafika!. Lakini ninyi mmeweza kufikisha huduma sehemu hizo! Juhudi hizo za kuunga mkono Serikali zimechangia sana nchi yetu kupiga hatua kubwa katika kusogeza huduma muhimu za jamii karibu zaidi na wananchi katika maeneo mbalimbali. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nanyi pamoja na madhehebu mengine yote ya dini katika kuboresha maisha ya Watanzania. Aidha, tutaendelea kupokea ushauri wenu na kuwashirikisha katika mambo mbalimbali yanayohusu sera, mipango na mikakati ya maendeleo ya nchi yetu na watu wake ikiwa ni pamoja na maeneo ya kipaumbele na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili. Nanyi, kwa upande wenu, tunawaomba muendelee kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwekeza katika maeneo mbalimbali ili kukuza uwezo wa BAKWATA. Aidha, muendelee kutumia mtandao wenu wa kutoa huduma ambao upo nchi nzima kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Lengo letu libaki kuwa moja, yaani tufanye kazi pamoja, kwa kushirikiana, ili tufanikiwe zaidi.
Mheshimiwa Mufti,
Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Mkutano huu unatupa fursa ya kutafakari pamoja maendeleo ya Uislam na Waislam hapa nchini na pia kujikumbusha mambo muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu kwa ujumla. Hapa naomba nigusie kwanza suala la kudumisha amani ambalo ni muhimu kwa maendeleo yetu. Bahati nzuri, amani ni msingi muhimu katika dini ya Kiislam. Kama sikosei, Islam maana yake ni amani. Hata katika kusalimiana, Waislamu hutumia zaidi Assalam Aleykum, wakitakiana amani. Hivyo, dini ya Kiislam imejengwa katika tunu ya amani. Bila amani hakuna furaha wala maendeleo katika nchi. Ndiyo maana Waasisi wa nchi yetu na Wazee wetu waliweka msisitizo mkubwa katika kutunza na kulinda amani katika Taifa letu. Hivyo, sisi nasi hatuna budi kuenzi na kuitunza amani yetu kwa manufaa yetu tunaoishi sasa na vizazi vijavyo. Kwa sababu hiyo, nichukue fursa hii kuwaomba viongozi wetu wa dini na wajumbe wa Mkutano huu kuongeza juhudi kuwaelimisha vijana, waumini na wanachi wetu kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kulinda amani, upendo, umoja na kuhimiza udugu na mshikamano miongoni mwa Watanzania wote. Kamwe tusiruhusu watu wachache kuvuruga amani na umoja wetu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hili la kutafuta na kulea amani, Serikali inapenda kuwapongeza sana Viongozi wa dini wanaokutana chini ya mwavuli wa Kamati ya Amani Kitaifa na katika Mikoa ili kujenga maelewano na amani. Hili ni jambo jema sana lenye kuleta heri katika nchi yetu ya Tanzania. Nashawishika kuwaomba muendeleze utaratibu huu mzuri na hata mpeleke wazo la kuanzisha utaratibu huu nchi jirani hasa zile ambazo bado hakuna amani ya kudumu. Aidha, ninawaomba muangalie uwezekano wa kuchapisha mada zilizotolewa kwenye kongamano la Viongozi wa Dini lililofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma tarehe 17 Aprili, 2021.
Jambo la pili ni kuhusu maadili mema. Naomba ninyi Viongozi wetu wa dini mwendelee kwa nguvu zaidi kulea nchi yetu kimaadili na kukemea maovu. Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia vitendo vinavyoashiria mmomonyoko mkubwa wa maadili. Vitendo viovu na mambo yasiyoipendeza jamii na yasiyompendeza Mwenyezi Mungu bado yapo katika jamii zetu. Mambo ambayo siku za nyuma yalikuwa nadra sana kutokea au kusikika sasa yanakuwa habari za kawaida na wakati mwingine huonekana ati ndiyo utaratibu. Mathalan: Watoto kutokuheshimu wakubwa, wazee kutokujiheshimu, ubakaji, ulevi, rushwa na ufisadi, uvivu, ujambazi na wizi ikiwa ni pamoja na kupora fedha na mali za wahanga wa ajali za barabarani na kushamiri kwa biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Hivi ni vielelezo dhahiri vya uwepo wa mambo yasiyokubalika kimaadili katika jamii yetu. Kuporomoka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Kunachangia sana kurudisha nyuma juhudi za kuharakisha maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mimi naamini kwa dhati kuwa watu wakishika mafundisho ya dini zao vizuri, maovu mengi yatapungua sana. Ndiyo maana narejea ombi langu ninalolitoa mara kwa mara kwa viongozi wa dini zote, mara ninapopata fursa kama hii, kwamba muisaidie Serikali kujenga jamii yenye maadili mema. Tuweke mkazo zaidi kwa vijana kwa sababu, kwanza wao ndio walengwa wakuu wa maovu yanayotendeka. Lakini pili, wao ndio Taifa la leo na kesho, ndio warithi wa Taifa letu. Tukiwaandaa vyema, mustakabali wa Taifa letu na watu wake utakuwa kwenye mikono salama. Tukishindwa leo, tutalia na kusaga meno kesho na Taifa letu litakuwa mashakani.
Mheshimiwa Mufti,
Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Suala la tatu ni muhimu wa kuiombea nchi yetu na Viongozi wake. Naomba pia niseme kwa dhati kabisa kwamba sisi tuliopo Serikalini tunategemea sana maombi yenu ili kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi. Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru sana viongozi na waumini wa dini zote nchini kuendelea kumuombea dua njema Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake yote. Dua zenu zinatuimarisha na kutupatia hamasa ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi na uadilifu. Nawaombeni mzidi kuliombea Taifa letu na Viongozi wake ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea. Dira na muelekeo wa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya. Hivyo maombi yenu ni muhimu sana katika kutuwezesha kutimiza wajibu wetu ili kufikia hayo malengo tuliyojiwekea.
Jambo la nne linahusu wananchi kufanya kazi halali kwa bidii na maarifa. Tunawaomba muendelee kuwahimiza waumini wa dini zetu na wananchi kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo. Uvivu ni adui mkubwa wa maendeleo. Tusipofanya kazi hatuwezi kupunguza umaskini. Kuna usemi usemao “kazi ni kazi tu”! Mimi msisitizo wangu ni kufanya kazi zilizo halali kujipatia kipato. Tanzania ni ya Watanzania! Hakuna Taifa au watu wengine watakaokuja kuleta maendeleo hapa nchini. Tufanye Kazi na wakati huo huo tukimtanguliza Mola wetu katika kila jambo. Bahati nzuri nchi yetu inazo fursa nyingi katika sekta mbalimbali (kilimo, ufugaji, uvuvi, uongezaji thamani wa bidhaa zinazozalishwa, uchimbaji wa madini, biashara na utoaji wa huduma mbalimbali. Hata ustadh wanaofundisha dini ni fursa pia!)
Mheshimiwa Mufti,
Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Eneo la tano ninalopenda kusema hapa ni umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Nchi yetu imeendelea kukumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimesababishwa na ongezeko la gesijoto, hasa hewa ya ukaa (Carbon dioxide) angani. Ongezeko la gesijoto linasababishwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu, ikiwemo moshi/gesi zinazotoka viwandani na ukataji wa miti hovyo. Athari ambazo tayari zimeshajitokeza ni pamoja na ukame wa muda mrefu, mafuriko, kuongezeka kwa ujazo wa bahari/maziwa kunakopelekea baadhi ya visiwa kuzama, kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza na kubadilika kwa mifumo ikolojia. Sote tunashuhudia kuwa athari hizo ni kubwa na zimedhihirika kuenea katika maeneo mengi duniani na hata hapa nchini. Athari hizo zimechangia ongezeko la majanga ya asili hususan katika nchi zinazoendelea kama Tanzania ambazo uwezo wake wa kuhimili majanga haya ni mdogo.
Nafahamu BAKWATA imekuwa ikiongoza mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya mazingira, hasa mashuleni. Niwaombe kupitia mkutano huu, muendelee kutusaidia kuwaelimisha waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi wote juu ya suala zima la kutunza mazingira, upandaji miti na matumizi bora na endelevu ya maliasili zetu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mufti,
Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Jambo la sita ni tahadhari kuhusu ugonjwa wa CORONA. Kuanzia mwishoni Mwaka 2019 Dunia ilikumbwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19). Ugonjwa huu sio janga la kiafya pekee bali ni janga la kiuchumi pia kwani limeambatana na kuvurugika kwa mfumo wa uzalishaji wa bidhaa na huduma na pia uhitaji katika nchi nyingi ikiwemo nchi yetu. Niwaombe sana ninyi Viongozi wetu kuwahimiza wananchi wote, tukianzia na familia zetu, kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu wetu wa afya. Ni muhimu sana kusisitiza kunawa maji kwa sabuni mara kwa mara, kuvaa barakoa katika maeneo yenye msongamano wa watu na kuacha nafasi ya kutosha kati ya mtu na mtu. Taarifa zilizopo ni kuwa nchi mbalimbali pamoja na nchi yetu zinaweza kukumbwa na wimbi la tatu la COVID-19. Hivyo, lazima tuchukue tahadhari pamoja na kumuomba Mola wetu atuepushe na wimbi hilo, kama alivyotuepusha na Kimbunga Jobo.
Mheshimiwa Mufti,
Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Jambo la saba ni kuhusu migogoro katika taasisi za kidini. Katika maelezo ya utangulizi, Katibu Mkuu wa BAKWATA amezungumzia suala la uwepo wa migogoro mbalimbali katika Taasisi za Dini. Tayari nimezungumzia kuhusu umuhimu wa pekee wa kudumisha amani na nimesisitiza kwamba amani ni chachu ya maendeleo. Hakuna maendeleo bila amani. Migogoro ni chanzo cha kurudisha nyuma maendeleo.
Nawasihi sana BAKWATA, Viongozi wote wa dini ya Kiislam na dini nyingine na pia Wakuu wa Taasisi zote za Dini kujitahidi kuziendesha Taasisi hizo kwa mujibu wa Katiba zao na mafundisho ya Dini. Naamini Taasisi zote za Dini zilizosajiliwa zinaendeshwa kwa kufuata Katiba ambazo wamesajiliwa nazo. Isitoshe, Taasisi za Dini zina mafundisho yake mahususi na miongozo yenye misingi katika Vitabu vya Dini hizo. Naamini tukizifuata Katiba na miongozo hiyo, tutaepuka migogoro. Naomba niseme tena hapa kwamba, Serikali imechoshwa na migogoro katika taasisi za kidini kwa kuwa inawagawa na kuwakwaza waamini katika imani zao. Migogoro inakwamisha maendeleo na wakati mwingine hata kuhatarisha amani katika nchi. Niwaombe sana BAKWATA ambaye ni mlezi wa taasisi hizi kwa upande wa dini ya Kiislam, kuzisimamia taasisi hizi kwa haki ili kuepusha migogoro isiyokuwa na tija.
Mheshimiwa Mufti,
Wajumbe wa Mkutano Mkuu;
Ninapokaribia kuhitimisha hotuba yangu niwaombe tena viongozi wa BAKWATA Mhakikishe mnaipigania na kuilinda amani kwa kila hali, ikiwa ni pamoja na kupambana na viashiria vya uvunjifu wa amani. Dini ni taasisi muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku, ndio maana Serikali inaheshimu na kuzitambua dini zote kutokana na mchango wake mkubwa katika kudumisha amani ya nchi yetu. Niwaombe viongozi wangu, popote mlipo, muilinde amani yetu. Aidha, ninawaomba Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) msichoke kuendeleza jitihada za kuwaunganisha waislamu wote bila ya kujali madhehebu yao au rangi zao.
Mwisho kabisa napenda kusema mambo mawili mafupi; Kwanza, nimewaletea fedha kidogo kutoka kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili wajumbe wa mkutano mkuu huu wa BAKWATA wapate japo maji ya kunywa. Pili, naomba kukushukuru tena Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania kwa kunialika ili nishiriki kwenye Mkutano huu muhimu. Nakushuru sana kwa heshima hii kubwa mliyonipatia. Baada ya kusema haya sasa natamka kuwa MKUTANO MKUU WA BAKWATA SASA UMEFUNGULIWA RASMI.
Wabilah Tawfik, Wahadha, Assalam Aleykum!
Mungu Ibariki Tanzania
Asanteni Sana kwa kunisikiliza!