Mtaalamu wa maabara wa Hospitali ya KAM Musika ya Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam, Rosemary Shirima, akimtoa damu mmoja wa watu waliofika kwenye hospitali hiyo kwaaajili ya kupata huduma za bure za vipimo na matibabu kwenye kambi ya siku tatu ya kutoa matibabu bure ambapo watu 1,500 walipatiwa huduma hiyo.
Mkurugenzi wa KAM Musika Hospital, Dk Kandore Musika akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye hospitali hiyo Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam kwaajili ya kupata huduma za bure za vipimo na matibabu hospitalini hapo ambapo wagonjwa 1,500 walipata huduma ya vipimo na tiba.
Mkurugenzi wa KAM Musika Hospital, Dk Kandore Musika akizungumza na mmoja wa watu waliokwenda kupata huduma hizo za bure kwenye hospitali hiyo eneo la mapokezi ya hospitali hiyo iliyoko Kimara Korogwe jijini Dar es Salaamambapo watu zaidi ya 1,500 walipata huduma hiyo.
*****************************
Na Mwandishi Wetu
WATU zaidi ya watu 1,500 wamejitokeza na kupata huduma za bure za vipimo na matibabu katika hospitali ya KAM Musika kwa muda wa siku tatu ikiwa ni mpango wake wa kusaidia jamii.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa hospitali ya KAM Musika, Dk. Kandore Musika kwenye kambi maalum ya matibabu bure kwa wananchi mbalimbali.
Hospitali hiyo iliyoko Kimara Korogwe iliendesha kambi ya siku tatu ambapo zaidi ya watu 1,500 walichunguzwa afya zao na kupatiwa matibabu bila malipo.
Dk. Musika alisema kwa kuwa hospitali hiyo ni mpya imejielekeza kutoa huduma zaidi kwa wananchi badala ya kuangalia biashara kwani watanzania wengi hawawezi kumudu gharama za vipimo na matibabu.
Alisema kila mwaka Hospitali ya KAM Musika itakuwa ikitenga wiki maalum kwa watanzania kwenda kufanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu bure kama sehemu ya mchango wake kwa jamii.
Alisema kwenye kambi hiyo wamepima na kuwabaini watu mbalimbali wenye magonjwa kama UTI, Malaria, kuhara, sukari, shinikoizo la damu na maradhi mbalimbali ya macho.
“Ni vizuri sana kupima mara kwa mara kujua afya yako ili uweze kutibiwa kabla hali haijawa mbaya sana kwa mfano kwenye hii kambi tumegundua watu wengi wenye sukari na shinikizo la damu ambao walikuwa hawajui sasa hii ni mbaya sana kwa afya,” aliasa Dk. Musika
Alisema KAM hospital itajitahidi kuwasaidia watanzania kwa kuhakikisha inawahudumia kwa gharama nafuu za vipimo na matibabu ili wengi wajitokeze kupima afya zao na kutibiwa.
Alisema ili kuepukana na maradhi mbalimbali pia wananchi wanashauriwa kula chakula chenye mlo kamili wenye protini, vitamin na wanga ili kuhakikisha wanakuwa na afya bora.
Alisema wanapaswa pia kusafisha mazingira ya kuishi kuhakikisha hakuna maji yanayotuamana ambayo hutengeneza mazalia ya mbu na kusababisha maradhi yaa kuhara na kichocho.
Mmoja wa wanufaika wa matibabu hayo, Ndumaeli Ulomi aliishukuru hospitali ya KAM kwa kutoa vipimo na matibabu ya bure akisema kuwa si watanzania wote wanamudu huduma hizo.
“Tunaomba wengine nao waige mfano huu kwasababu watanzania wengi wanashida ila hawana uwezo wa kugharamia vipimo na matibabu tunawashukuru sana na waendelee na moyo huu wa kuwasaidia watanzania,” alisema
Scarion Marcel ambaye naye alinufaika na huduma hizo za bure, aliishukuru Hospitali ya KAM kwa kutenga wiki ya huduma bure za vipimo na matibabu kwani watanzania wengi wasio na uwezo wamenufaika na huduma hizo.
“Kwa kweli hii inastaajabisha kuona hospitali inajitolea kuchunguza wagonjwa na kuwatibu bure iwapo watanzania wengi watakuwa na moyo kama huu nchi itafika pazuri kwasababu watu wengi wasio na uwezo watanufaika,” alisema
Mwisho