*******************
Jumla ya wagombea kumi na mbili (12) wamechukua fomu za uteuzi kwa ajili ya kuwania ubunge kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Konde, Kisiwani Pemba unaotarajiwa kufanyika tarehe 18 Julai, 2021.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Konde, Yasini Jabu Hamis amesema kwamba wagombea hao wanatarajiwa kurejesha fomu kabla ya saa 10:00 jioni tarehe 27 Juni, 2021 kwa ajili ya uteuzi.
Wagombea waliochukua fomu wanatoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Civic United Front (CUF), Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Sauti ya Umma (SAU), National Convention for Constitution and Reconstruction-Mageuzi (NCCR-Mageuzi), Tanzania Labour Party (TLP), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Demokrasia Makini, Chama cha Kijamii (CCK), United People’s Democratic Party (UPDP), National Reconstruction Alliance (NRA) na Tanzania Democratic Alliance (ADA-TADEA).
Jimbo la Konde linafanya uchaguzi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Khatib Said Haji. Uchaguzi huo unafanyika sambamba na kata sita (6) za Tanzania Bara, ambazo ni Mbagala Kuu iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam (Temeke), Ndirigish iliyopo Mkoa wa Manyara (Kiteto), Mitesa na Nchemwa zilizopo Mkoa wa Mtwara (Masasi na Newala), Gare iliyopo Mkoa wa Tanga (Lushoto) na Chona iliyopo Mkoa wa Shinyanga (Ushetu).
Kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo zinatarajia kuanza tarehe 28 Juni, 2021 hadi 17 Julai, 2021 na uchaguzi unatarajiwa kufanyika tarehe 18 Julai 2021.