Wadau mbalimbali wa chakula wakiwa katika mkutano wa pamoja katika mjadala huo uliolenga kujadiliana maswala mbalimbali ikiwemo changamoto zinazowakabili (Happy Lazaro)
Wadau mbalimbali wa maswala ya chakula wakiwa katika picha ya pamoja katika mjadala wa mfumo wa chakula Kanda ya kaskazini uliofanyika mjini hapa (Happy Lazaro)
*********************************
Happy Lazaro, Arusha
Wadau mbalimbali wanaojihusisha na minyororo ya thamani katika mifumo ya chakula kutoka Kanda ya kaskazini wamekutana jijini Arusha katika kujadili changamoto zinazowakabili na kuweza kuziboresha kwa kufikia malengo yaliyowekwa.
Akizungumza katika ufunguzi wa mjadala wa mifumo ya chakula Kanda ya kaskazini,Meya wa jiji la Dodoma ,Profesa Davis Mwamfupe amesema kuwa,mjadala huo umewajumuisha wadau wa mifumo ya chakula ambao ni wazalishaji wa chakula,wasindikaji,wasafirishaji, wafanyabiashara wa kilimo pamoja na walaji ili kuweza kuainisha njia kabambe zenye kutengeneza mifumo ya chakula imara na yenye usawa zaidi,na hatimaye kuleta maendeleo kwa haraka.
Amesema kuwa,mfumo wa chakula una mafungamano na changamoto zilizoenea duniani ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa ,magonjwa sugu,magonjwa yasiyo ya kuambukiza,ukosefu wa usawa wa kijamii,madhara ya ustawi wa wanyama, uharibifu wa mazingira, na nguvu za kiuchumi ambapo mambo hayo yanaweza kuathiri upatikanaji wa matumizi ya chakula.
Profesa Mwamfupe amesema kuwa,kupitia majadiliano hayo wataweza kupata maoni na kujua changamoto mbalimbali kutoka kwa wadau na hivyo kutoa mapendekezo nini kifanyike katika kuboresha maswala hayo ili kuleta maendeleo kwa haraka na kufikia malengo yote 17 ya maendeleo endelevu ya umoja wa Mataifa .
“Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimetia saini makubaliano ya kutekeleza malengo 17 ya maendeleo endelevu ya umoja wa Mataifa ifikapo 2030 ,ingawa nchi zimefanya jitihada mbalimbali za kufikia malengo hayo,lakini wengi wao hawajaweza kuyafikia malengo yaliyowekwa”amesema Profesa Mwamfupe.
Ameongeza kuwa,mwaka 2019 ,Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa alitoa wito wa kuwa na mijadala ya mifumo ya chakula na kuanzisha mchakato wa ushirikishaji ili kubainisha namna ambavyo mifumo ya chakula inaweza kuboresha ili kuleta maendeleo kwa haraka na kufikia malengo yote 17 ya maendeleo endelevu ya umoja wa Mataifa .
Naye Mratibu wa Mviwata mkoa wa Arusha, Richard Masandika amesema kuwa,kupitia mjadala huo unalenga kuangalia changamoto ya uzalishaji katika maswala ya chakula na mazingira pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi sambamba na ubunifu katika mabadiliko ya chakula.
Amefafanua kuwa,mwisho wa mjadala huo wataweza kupata mapendekezo yanayotokana na maswali mbalimbali waliyoyajadili na yatapelekwa serikalini.
Naye Mkurugenzi wa idara ya usalama wa chakula katika wizara ya kilimo,Dokta Honest Kessy amesema kuwa,wanafanya mijadala ya kutafakari namna ya kuboresha mifumo ya chakula katika Kanda ya kaskazini ikiwa na lengo la kuangalia mnyororo mzima wa uzalishaji mpaka kumfikia mlaji.
Ameongeza kuwa ,kupitia mjadala huo wanaweza kuangalia kwa sasa hivi wanapofanya uzalishaji na usindikaji wao wanaangalia kuna changamoto gani ambazo wangependa kuzitatua sambamba na kuangalia huo mfuko una malengo gani,hasa kwa kusikiliza mawazo ya wakulima na wafugaji ili waweze kusema kwa hali ilivyo sasa hivi wana matamanio gani.
“Mijadala hii itaendeshwa nchi nzima ili iweze kuwafikisha katika malengo 17 endelevu ya umoja wa kimataifa yanayolenga kuondoa umaskini na njaa katika jamii ambapo yatafanywa katika ngazi ya kitaifa, kimkoa na kikanda ambapo mapendekezo hayo yatawasilishwa katika mkutano wa umoja wa Mataifa utakaofanyika mjini New work Marekani ,mwezi septemba ,2021,ambapo hiyo itasaidia kupunguza umaskini kwa wananchi wake na kuondokana na hali ya kutokuwa na njaa.”amesema Dokta Kessy.