Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akihutubia Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Shinyanga mapema jana makao Makuu ya Wilaya hiyo Iselamagazi Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko wakiwasili katika ukumbi wa Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Shinyanga mapema jana makao Makuu ya Wilaya hiyo Iselamagazi Shinyanga.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Madiwani la Wilaya ya Shinyanga wakifuatilia jambo kwa makini wakati wa kujadili hoja za ripoti ya mkaguzi wa hesabu serikali jana.
…………………………………………………………………..
Na Anthony Ishengoma -Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati amesema ataendelea kuchukua hatua kwa viongozi na watumishi wazembe wanaofanya kazi kwa mazoea na kusababisha hati chafu baada ya kukamilika kwa ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali.
Dkt. Sengati amesema hayo jana wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Shinyanga kilichofanyika katika Makao Makuu ya Wilaya hiyo Iselamagazi Shinyanga na kusisitiza kuwa atatekeleza suala hilo bila kuhurumia mtu yeyote.
‘’ Itakuwa fedhea kubwa sana kupata tena hati chafu, itakuwa atutendei haki wanashinyanga,itakuwa hatutendei haki nafasi zetu haya madhara yake ni mabaya kwasababu hata wawekezaji wataogopa kuja wataona sio salama kuwekeza.’’Aliendelea kusisitiza Dr. Sengati.
Akiongea kwa uchungu mkubwa Dkt. Sengati aliongeza kuwa katika Mkoa wa Shinyanga wako Weka Hazina wabovu kweli kweli na aliwahakikishia wajumbe wa baraza la madiwani kuwa wasipojirekebisha atawachukulia hatua za kinidhamu za kiutumishi akisisitiza kuwa baadhi yao watapoteza kazi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko aliendelea kupigilia msumari wa moto kwa watendaji hao wazembe kwa kusema kuwa suala la hati chafu limekuwa likijitokeza kutokana na baadhi ya watendaji hao wazembe kutochukuliwa hatua na kumtaka Mkuu wa mkoa kuahakisha wanawajibishwa ili kuboresha utendaji kazi.
Aidha Bi. Jasinta Mboneko ameonya tabia ya watendaji wanaokusanya fedha serikali kuacha tabia ya kukaa na fedha bila kuzipeleka Benki akionya kuwa sula hilo pia linachangia sintofahamu katika suala zima la hesabu za serikali na kuagiza wale wote wanaousika kuacha tabia hiyo mara moja.
Mwenyekiti wa Baraza la madiwani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shinyanga Bw. Ngasa Mboje wakati akihitimisha kikao chake alionesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa TEMESA na kudai kuwa wakala huyo wa Serikali amekuwa akiwasilisha madai makubwa ya matengenezo ya magari jambo linachangia kukwamisha utendaji kazi.
‘’Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ina mapato madogo sana Wakala wa Serikali TEMESA anawasilisha kwetu kiasi cha Tsh. M.18 kwa matatizo ya kawaida ya magari na kusabaisha gari kukaa muda mrefu bila matengenezo hapo kweli tutawafikia wananchi. Aliongeza Mwenyekiti wa Baraza hilo.’’ Bw. Ngasa Mboje.
Baraza la Madiwani Wilaya ya Shinyanga limekutana kwa siku moja jana kujadili hoja mbalimbali zilizojitpokeza katika ripoti ya mdhibiti na mkaguzi wa hoja serikali ambazo zilipelekea halmashauri kupata hati chafu.