******************************
20, Juni 2021-Lindi
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (MB) amekutana na wadau wa mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (Liquefied Natural Gas-LNG) katika mkutano uliofanyika Mkoani Lindi kwa lengo la kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo.
Akizungumza na wadau, Waziri Kalemani alieleza kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuteleleza mradi wa LNG na tayari kazi mbalimbali zimekwishafanyika ikiwemo utwaaji wa ardhi ya mradi yenye ukubwa wa hekta 2,071, ulipaji wa Bilioni 5.7 kama fidia kwa wananchi watakaopisha mradi, upembuzi wa awali wa kihandisi (Pre FEED) pamoja na kuundwa kwa Timu ya Serikaki ya Majadiliano (Government Negotiation Team-GNT) na Timu ya Wataalam (Technical Team) itakayofanya kazi na GNT.
Waziri Kalemani alieleza kuwa Serikali imejipanga kukamilisha majadiliano ya Mkataba wa Nchi Hodhi (Host Governmemt Agreement-HGA) ndani ya miezi 6 ili kuwezesha utekelezaji wa mradi kuanza mapema, “kufikia mwezi wa kumi majadiliano ya HGA yatakuwa yamekamilika” alieleza Waziri Kalemani. Waziri Kalemani pia aliilekeza TPDC kukamilisha ndani ya mwezi mmoja zoezi la uwekaji wa mipaka katika eneo la mradi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alieleza sababu zilizopelekea mradi kuchukua muda mrefu ambazo ni pamoja na zoezi la upitiaji wa mikataba ambapo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliiagiza Serikali kufanya mapitio ya Mikataba ya Ugawanaji Mapato (Production Sharing Agreement- PSA). Zoezi la kupitia Mikataba ya PSA lilitekelezwa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na lilipelekea majadiliano yaliyokuwa yameanza mwaka 2016 kusimama kupisha zoezi hilo muhimu kukamilika, alieleza zaidi Dkt. Mataragio.
Nae Mkuu wa Wilaya Mteule wa Lindi, Ndg. Shaibu Ndemanga aliemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi katika kikao hicho alieleza kufurahishwa kwake kwa namna ambayo TPDC imekuwa ikiwashirikisha wadau wa LNG Lindi kwa kuwapa taarifa za mara kwa mara jambo ambalo liliondoa sintofahamu juu ya mradi huu. Ndg. Ndemanga pia alisema “kipekee niwashukuru Wizara ya Nishati na TPDC kwa namna ambayo walishughulikia zoezi la fidia kwa waathirika wa mradi wa LNG ambapo wananchi walifuatwa katika maeneo yao na hivyo kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata haki yao”
Mkutano wa Wadau wa mradi wa LNG ulihudhuriwa na Wabunge wa Lindi na Mtwara, Wafanyabishara wa Lindi, Wawakilishi wa wawekezaji kutoka kampuni za Shell na Equinor, Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Lindi na watumishi wa Wizara ya Nishati na wale wa TPDC
Mradi wa LNG unatarajiwa kutekelezwa katika Mkoa wa Lindi, Manispaa ya Lindi, Kata ya Mbanja katika mitaa ya Likong’o, Mto Mkavu na Masasi ya Leo. Uwekezaji katika mradi huu unaelezwa kufikia hadi Dola za Marekani Bilioni 30 na utatekelezwa na Serikali kupitia TPDC kwa upande mmoja na wawekezaji ambao ni Kampuni za Shell na Equinor pamoja na washirika wao kwa upande mwingine. Mradi huu utawezesha gesi asilia iliyogundulika katika kina kirefu cha maji baharini (futi za ujazo trilioni 47.08) kuweza kuvunwa kibiashara ambapo sehemu ya gesi hiyo itauzwa soko la kimataifa katika nchi za Asia na nyinginezo na kiasi kingine kitatumika kwa matumizi ya ndani ya nchi pamoja kanda.