************************
Na John Mapepele, Mtwara
Wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya, wakiongozwa na Maua Sama na Chegi wamekonga nyoyo za wanamichezo wa UMISSETA na kuleta hamasa kubwa kwa wanamichezo na wadau mbalimbali wa mkoa wa Mtwara walipotumbuiza jukwaani leo Juni 2021 kwenye ufunguzi wa Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yaliyofunguliwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Caroline Nombo kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Katika ufunguzi wa leo wa UMISSETA vikundi mbalimbali vya kwaya na ngoma vimetumbuiza na kuufanya umati wa watazamaji kupanda jukwaani na kuimba pamoja na wasanii mbalimbali waliokuwa wakitumbuiza.
Akisoma hotuba ya ufunguzi wa mashindano hayo Profesa Nombo amepongeza ubunifu wa waandaji wa mashindano ya mwaka huu kwa kuwashirikisha wasanii ili kuja kutoa burudani katika kipindi cha mashindano haya na kuonesha vipaji na vipawa walivyopewa na Mwenyezi Mungu.
“Pia ninawashukuru na kuwapongeza wasanii mbalimbali wanaoendelea kusherehesha wakiwemo Maua Sama na Chege. Wanahabari na wasanii hawa wanasaidia kuitangaza michezo hii na wameongeza hamasa kwa jamii kuifuatilia nchi nzima wakiwemo wazazi, walezi wa wanafunzi na Viongozi wa Vyama vya Siasa na viongozi wa Serikali popote walipo”. Aliongeza Profesa Nombo
Profesa Nomba alitumia ufunguzi wa mashindano haya kuwaagiza wadhibiti ubora wa Shule kote nchini kuanzia ngazi ya wilaya, kanda na Makao makuu ya Wizara kufanya tathmini na kutoa ushauri wa kuimarisha ufundishaji wa michezo, elimu kwa michezo na sanaa katika taasisi zote hapa nchini
Amesema katika kipindi hiki Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa shule zinatenga maeneo maalum kwa ajili ya michezo na Sanaa ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi.
Amesisistiza kuwa michezo ya UMISSETA na ile ya vyuo vya ualimu (UMISAVUTA) imekuwa ikiibua vipaji vya wanamichezo wengi ambao miongoni mwao wamefanikiwa kung’ara kitaifa na kimataifa ambapo amesema kutokana na hilo Serikali imeamua kurejesha mashindano yaVyuoi vya Ualimu pia kwa kuzingatia agizio la Mkuu alilolitoa mwaka 2019 wakati wa kufungua mashindanio ya UMISSETA na UMITASHUMTA la kutaka mashindano hayo yarejeshwe.
Aidha amesema wachezaji wenye mafanikio duniani ni wale wenye nidhamu viwanjani na nje ya uwanja na kuwataka wanamichezo wote kuwa na nidhamu ili kufika katika kiwango cha juu.
“ Mfano wa wachezaji hao ni Mbwana Samatta, Hashimu Thabiti, Saimoni Msuva, Usain Bolt Lionel Messi, Christian Ronaldo na wengine wengi . ni matarajio ya kila mmoja wetu kuona mkishindana kwa ujuzi na maarifa ya hali ya juu ili kupata washindi mahiri wenye vigezo vya kuweza kushindana kitaifa na kimataifa” alifafanua
Mashindano yameandaliwa na Wizara tatu zinazohusika na Elimu, Michezo na TAMISEMI chini ya Kamati ya Uratibu ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.
Mashindano haya yalitanguliwa na Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Juni 8, mwaka huu mjini Mtwara na kufungwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekul Juni 18, 2021.Mashindano ya UMISSETA yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 3, mwaka huu.