Shujaa wa Yanga katika Mchezo wa Leo dhidi ya Mwadui FC Mshambuliaji Wazir Junior akiwa na wachezaji wenzake wakishangilia bao la ushindi alilolifunga dakika ya 90+3 na kuipa Yanga ushindi wa mabao 3-2.
Kiungo Mkabaji wa Yanga Mukoko Tonombe akijaribu kumtoka mchezaji wa Mwadui FC.
Winga wa Yanga Tuisila Kisinda akimpiga chenga mchezaji wa Mwadui FC
………………………………………………..
Na.Emmanuel Mbatilo,Dar es Salaam.
Mabingwa wa kihistoria Tanzania bara Timu ya Yanga imeendelea kuifukuzia Simba katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kutoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya vibonde Mwadui FC mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mwadui FC walikuwa wa kwanza kuliona lango la Yanga dakika ya 7 bao likifungwa na Aniceth Revocatus ,beki wa Yanga Bakari Mwamnyeto aliisawazishia timu yake dakika 21 akimalizia pasi ya Saido Ntibazonkiza.
Yanga walikosa Penalti dakika ya 43 baada ya golikipa wa Mwadui kucheza Penalti ya Fiston Abdul Razak mpaka mapumziko timu zote zilikuwa zimefungana 1-1 na kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ya wachezaji.
Mwadui waliandika bao la pili dakika ya 65 likifungwa na yule yule Aniceth Revocatus kwa shuti kali lililomshinda Farouk Shikalo.
Dakika nne za nyongeza zimetosha kuipa Yanga ushindi wa mabao 3-2,Mabao yakifungwa na wachezaji walioingia kipindi cha pili Yacouba Songne dakika ya 90+2 na Wazir Junior dakika ya 90+3
Kwa Matokeo hayo Yanga wanaendelea kubaki nafasi ya pili kwa Pointi 67 huku Simba wakiendelea kuongoza Ligi kwa Pointi 70 na Mwadui FC ambao wameshashuka daraja wanaendelea kukamilisha ratiba ya Ligi.