…………………………………………………………
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amesisitiza mambo mbalimbali ya kutiliwa mkazo na serikali katika utekelezaji wa bajeti yake ya 2021/2022 ikiwemo sekta ya kilimo kwak uwasaidia wakulima walime kilimo cha kisasa.
Aidha,ameiomba serikali kutekeleza miradi ya kimkakati katika wilaya ya Ikungi ikiwemo stendi ya mabasi na soko la kisasa.
Akichangia bajeti hiyo Juni 17 bungeni ,Mtaturu amesema kilimo kinachangia zaidi ya asilimia 26 ya fedha katika serikali lakini kiasi cha fedha kinachotengwa ni kidogo sana.
“Sote tunajua kwamba wananchi wengi wanajishughulisha na kilimo, maana yake ni kwamba shughuli kubwa inayofanywa na wananchi wetu ni kilimo lakini kilimo hiki kikitumika vizuri tukapata mazao ya kutosha tutaweza kupeleka malighafi nyingi kwenye viwanda na hivyo tutakuwa na uwezo mkubwa wa kukuza viwanda na kuongeza pato la Taifa,”alisema.
Kutokana na hilo ameiomba serikali kuongeza nguvu kwenye kilimo kwa kuwasaidia wakulima kulima kilimo cha kisasa ikiwemo kwenye zao la alizeti kutokana na zao hilo kulimwa katika mikoa 19 ikiwemo mkoa wa Singida.
“Nimpongeze Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,Juni 13 Mwaka huu aliitisha kikao cha wadau wa alizeti katika Mkoa wa Singida na alionyesha wazi kwamba serikali imedhamiria kuwekeza sana ili kuondokana na kuagiza mafuta nje ya nchi,”
Ameongeza kuwa kama nchi inatumia zaidi ya shilingi Bilioni 400 kila mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi ili kufidia upungufu wa mafuta ya kula nchini.
“Tumepata mwanga mzuri kwenye kikao hicho Waziri Mkuu alitumia saa nane kusikiliza maoni ya wadau ikiwemo yetu sisi wabunge,niombe kwenye eneo la kupata pembejeo litazamwe vizuri,fedha ziongezwe za mbegu ili wananchi walime alizeti itakayoleta mafuta mengi,”.
Amesema uzalishaji huo utasaidia upatikanaji wa mafuta mengi,utawezesha viwanda kuzalisha mafuta kwa mwaka mzima tofauti na ilivyo sasa viwanda vinazalisha miezi mitatu kutokana na kukosa mbegu za kukamua.
“Kama hii haitoshi tumeongelea habari ya upimaji wa udongo kuna maeneo mengi wakulima wanalima tu alimradi kutokana na kutojua ardhi yao ina uwezo gani wa kuzalisha mazao,tumeomba sana watafiti wetu wafanye kazi kuhakikisha kwamba ardhi tunayolima inakuwa ni ardhi inayojulikana wazi kama inahitaji mbolea ijulikane ni kiasi gani,”alisisitiza.
OMBI LA UJENZI WA SOKO NA STENDI.
Ili kuongeza mapato katika Halmashauri na serikali kwa kuu,ameomba kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa Soko na Kituo cha Mabasi.
“Wilaya ya Ikungi tulikuwa na maombi ya muda mrefu ya kuwa na kituo cha mabasi maana hatuna inayoweza kukidhi haja iliyopo katika wilaya yetu,pia tupate soko la kisasa ili kuongeza mapato ya halmashauri na hivyo kusaidia bajeti ya serikali kwenye kuleta maendeleo ya nchi yetu katika vijiji na halmashauri zetu,”aliomba.
MASLAHI YA WATUMISHI NA POSHO ZA MADIWANI.
“Niipongeze serikali kwa kuamua kuwapandisha madaraja watumishi wapatao 94,000, na nimeona zaidi ya Bilioni 400 zinaenda kufanya kazi hii,hili ni jambo jema sana, pamoja na kwamba tunasema hawaongezewi mishahara lakini ukipandishwa daraja una uhakika wa kulipwa mshahara kulingana na daraja lako,naomba sana wizara husika ihakikishe inasimamia vizuri wafanyakazi hawa wapate haki yao,”alisisitiza.
Kuhusu posho za madiwani ameipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kuwalipa posho hizo moja kwa moja kupitia hazina.
“Tunashukuru kwa hatua hii lakini huko nyuma kulikuwa na maombi ya muda mrefu ya kuongezwa kwa posho hizo,niiombe serikali iliangalie hili ili madiwani waendelee kufanya kazi nzuri,sisi tupo huku wao wanafanya kazi vijijini kule wapo karibu na wananchi wanasimamia maendeleo, tukiwaongezea wataongeza motisha na nguvu kubwa ya kusimamia maendeleo na fedha tunazopeleka kule,”aliongeza.
Pamoja na hilo ameiomba serikali kuongeza fedha kwa ajili ya kuwasaidia viongozi wa vijiji ili waweze kufanya kazi zao kwa tija.
AMPA TANO RAIS SAMIA .
Akizungumzia kuhusu bajeti hiyo kwa ujumla ameipongeza serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa bajeti nzuri inayomgusa mwananchi na iliyosikiliza kilio cha wabunge.
“Nampongeza Rais wetu,Jemedari wetu kwa kuendelea kuongoza vizuri nchi yetu na kwa namna ambavyo amekuwa akisikiliza maoni ya wabunge,miongoni mwa sifa inayompamba kiongozi ni kusikiliza watu wake,mama yetu anatusikiliza na anawasikiliza wananchi na anatuongoza vizuri,tunampongeza na kumtakia afya njema,
“Rais Samia amenyesha dhahiri kuwa hii ni bajeti ya kazi iendelee kwa sababu miradi yote ya kimkakati amesema itaendelea na juzi akiwa Mwanza amezindua tena ujenzi wa Reli ya SGR kutoka Mwanza hadi Isaka maana yake itakutana katikati iweze kukamilika ianze kufanya kazi,”alisema.
Amesema pongezi hizo zinatokana pia namna bajeti ilivyogusa maeneo yote muhimu hususan katika sekta ya miunddombinu ambapo kwenye barabara hasa za vijijini fedha zimetolewa kwa kila jimbo kiasi cha Shilingi Milioni 500.
“Hivi tunavyoongea mameneja wetu wa TARURA wanaendelea kufanya kazi ya kufanya maandalizi ya kujenga barabara zetu, maana yake barabara za vijijini zikiwa salama na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo kusafirisha mazao zitaenda kufanikiwa katika vijiji vyetu,
“Nimpongeze pia kaka yangu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba kwa kuwasilisha vizuri bajeti hii ambayo tunaijadili kwa hakika imejikita katika kutatua kero za wananchi, imeonyesha mwelekeo wa serikali kwa mwaka mmoja ujao,niwapongeze yeye pamoja na watendaji wake akiwemo Naibu Waziri na Katibu Mkuu,”alisema.