**************************
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo akiambatana na katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi Ndg. Shaka Hamdu Shaka na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Ndg. Ngemela Lubinga leo wameanza ziara ya siku nne Mkoani Tanga.
Msafara wa Katibu Mkuu ukiwa njiani kuelekea Tanga umesimamishwa na umati wa wanachama na wananchi kwa ujumla katika maeneo mbalimbali. Katika eneo la Mkata wilayani Handeni katika salamu, Katibu Mkuu ameeleza kuwa, ziara hiyo imelenga katika utatuzi wa chabgamoto za watu wote baada ya CCM kupata imani kubwa mwaka 2020.
“Tumekuja kushughulika na maendeleo na kutatua changamoto zenu, na hatutakuwa na maneno mengi. Kazi ya Chama chetu ilikuwa kuandaa Ilani na kuinadi mwaka 2020, Kazi tulikamilisha vizuri mkatupa ridhaa ya kuongoza nchi kwa miaka mitano, kazi yetu sasa ni kusimamia kile tulichoahidi tuone matokeo yake.” Ameeleza Katibu Mkuu.
Ziara hii ni ya kwanza kwa Katibu Mkuu na Sekretarieti Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, ikiwa ni mkakati wa kwenda mashinani kujenga na kuimarisha Chama.
Imetolewa na;
Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
11 Juni, 2021