Na Dotto Mwaibale, Singida
KAIMU Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani amewataka vijana mkoani Singida kuwa wabunifu katika kuendeleza miradi ya kiuchumi.
Ndahani ameyasema hayo juzi alipokuwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika Halmshauri ya Wilaya Mkalama na Singida ili kujionea shughuli za kiuchumi zinazofanywa na vijana walionufaika na mkopo wa mapato ya ndani ya halmashauri.
” Vijana wengi wanaanzisha miradi ya kiuchumi lakini hawapati mafanikio kulingana na matarajio hivyo kushindwa kurejesha mkopo kwa wakati,” alisema Ndahani.
Ndahani aliwaeleza vijana hao kuwa ubunifu katika biashara ni jambo la msingi katika kukuza biashara au shughuli yoyote ya kiuchumi,hivyo wanatakiwa kuwa wabunifu pamoja na kujifunza kwa waliofanikiwa.
Alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira rafiki kwa mashirika na asasi binafsi ili kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana ikiwemo kuwapatia mafunzo ya stadi za maisha na ujuzi,elimu ya ujasiriamali pamoja na masuala ya afya ya uzazi, hivyo vijana wanapaswa kuona fursa hii adimu na kuacha kulalamika na kuilaumu Serikali.
Alisema Mkoa wa Singida umejipanga kutekeleza sheria ya utoaji wa mikopo kupitia mapato ya ndani ili kuwapa vijana.
Aidha Ndahani aliwaomba viongozi wa vijana na mtaa kuwatengea maeneo vijana kwa ajili ya kuendeleza miradi yao ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara na viwanda kwa kufanya hivyo viongozi watakuwa wametimiza wajibu wao na kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa la kuvitaka vijiji,mitaa na halmshauri kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana.
Kwa upande wao vijana wa Mkalama na Wilaya ya Singida wamemshukuru Ndahani kwa kuwa karibu na vijana na kuiomba Serikali kuhimiza utoaji wa mikopo na mafunzo ili mikopo inayokopwa iendane na mahitaji ya vijana.
Afisa Maendeleo Vijana Wilaya ya Singida, Monica Nderike alimuhakikishia Ndahani kuwa ushauri uliotolewa kama halmshauri wataufanyia kazi ikiwemo kuwapatia mkopo wa vifaa badala ya fedha taslimu na kuongeza kasi ya utoaji wa mafunzo ya stadi za maisha na ujuzi.