**********************************
Nteghenjwa Hosseah, Dar es salaam
Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation, chini ya ufadhili wa wadau wa maendeleo hapa nchini, wamefanikiwa kuajiri Watumishi wapya wa Afya kwa kada mbalimbali 960 na watoa huduma za Afya Ngazi ya Jamii 1986 kwa mikataba ya kuanzia mwaka mmoja na kuendelea.
Akizungumza na vyombo vya habari Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI Dr. Grace Magembe kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha mchango huonwa wadau katika sekta ya Afya kwa kuwezesha upatikanaji wa Ajira za watumishi wa Afya ngazi ya Serikali za Mitaa.
Amesema ajira hizi zimezotolewa kwa mikataba ya kuanzia mwaka mmoja na kuendelea, ni tofauti na ajira 2720 za sekta ya Afya zilizotangazwa hivi karibuni kupitia agizo la Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Dr. Grace ameeleza kuwa Watumishi hao wameajiriwa kutoka katika kanzidata ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ikiwa ni waombaji wenye sifa wa ajira za Afya zilizotangazwa kipindi cha nyuma lakin hawakuweza kuajiriwa wote kutokana na ufinyu wa nafasi hizo.
‘Upatikanaji wa watumishi hawa ni sehemu ya mipango ya Serikali kwa kushirikiana na wadau kuweka mifumo imara ya utoaji huduma za afya kwa watanzania wote.
Idadi hii ya watumishi imekuja wakati muafaka ambapo Serikali inatekeleza vipaumbele vyake hususani katika kuhakikisha utoaji huduma bora katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza na sambamba na kuongeza nguvu ya kupambana na magonjwa ya mlipuko kama vile maambukizi ya Homa ya Mapafu (COVID – 9)’ alisema Dr.Grace.
Akizungumza katika kikao hicho Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation Dr. Ellen Mkondya Senkorona amesema wadau waliowezesha kuajiriwa kwa watumishi hao ni Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund), Shirika la UNICEF, Irish Aid na Foreign, Commonwealth and Development Office (FCDO) ambao wameipatia Tanzania fedha kupitia Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation ili iweze kuajiri watumishi hao.
Dr. Ellen ameongeza kuwa kiasi cha fedha zitakazotumika wakati wote wa ajira za watumishi hao kwa kulipa mishahara na stahiki zingine ni shilingi Bilioni 19.
Ajira hizi zimekuja wakati muafaka ambapo Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imejenga Hospitali za Wilaya 102, Vituo vya Afya 488 Zahanati 1198 na nyumba za watumishi 840 vituo vyote hivi vinahitaji watumishi wenye ujuzi na na weledi ili kuweza kutoa huduma bora.