Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipotoa tamko kuhusu wiki ya mazingira duniani kwenye ukumbi wa hazina jijini Dodoma, Juni Mosi, 2021.
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipotoa tamko kuhusu wiki ya mazingira duniani kwenye ukumbi wa hazina jijini Dodoma, Juni Mosi, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara, Taasisi, Mashirika yote ya Serikali na Sekta Binafsi na wakandarasi wanaosimamia ujenzi wa majengo nchini kuhakikisha yanawekewa mfumo maalum wa kupitisha gesi kama nishati mbadala kwa matumizi ya kupikia.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa maagizo hayo leo Juni 1,2021 jijini Dodoma wakati akitoa tamko la serikali katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika Juni 5 kila mwaka, ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Dodoma.
Pia Majaliwa ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuanzisha kampeni ya upandaji miti kwa maeneo yote yaliyopimwa, ambapo kila mmiliki wa kiwanja au nyumba atapaswa kupanda mti katika eneo lake.
Amesema kuwa taasisi kama shule, vyuo, hospitali na majengo makubwa zinapaswa kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia.
“Kila Wizara ifanye ufuatiliaji kwenye taasisi zake na nipatiwe taarifa ya hali ya utekelezaji kila baada ya miezi sita inayoonesha ni taasisi ngapi zimefikiwa, zimebadili mifumo au zimejenga majengo kwa kuzingatia hitaji la nishati mbadala”
“Suala la uhifadhi, utunzaji, usimamizi na usafi wa mazingira lisiwe jambo linalofanyika wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani pekee, bali tujenge tabia ya kuliona kwamba ni suala la kila siku” amesisitiza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo,amesema kuwa katika kuadhimisha siku ya Mazingira duniani zaidi ya Wadau wa Mazingira 100 wanashiriki ambapo Juni,4,2021 kutakuwa na kongamano la Mazingira na Juni 5,2021 ikiwa ni kilele cha siku ya Mazingira na kukiwa na kampeni kabambe ya Mazingira .
Jafo amesema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha jamii umuhimu wa utunzaji wa Mazingira na kuelimisha juu ya madhara yatokanayo na uharibifu.
“Kampeni haitoacha kitu. Tunataka kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya kupigiwa mfano katika utunzaji mazingira duniani,” amesisitiza