***************************
Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imefanya kikao chake cha kawaida cha 214 tarehe 28 Mei 2021. Katika kikao hicho kamati ilipitia utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia. Kamati iliridhika na utekelezaji wa sera ya fedha ambayo imewezesha kuwepo kwa ukwasi wa kutosha katika sekta ya benki, hivyo kuweza kutoa mchango kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi. Aidha, kuendelea kuwepo kwa mfumuko wa bei katika viwango vya chini kumeendelea kusaidia utekelezaji wa sera wezeshi ya fedha.
Kamati ya Sera ya Fedha imeridhishwa na mwenendo wa uchumi, licha ya kuwepo kwa changamoto zinazotokana na athari za Corona kwenye baadhi ya shughuli za kiuchumi. Kutokana na hali hii, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 4.8 mwaka 2020, pungufu ya matarajio ya ukuaji wa asilimia 5.5. Shughuli za kiuchumi zinatarajiwa kuimarika zaidi mwaka 2021, ambapo ukuaji wa uchumi unakadiriwa kufikia asilimia 5.6. Ukuaji huu utachangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, kilimo, uchukuzi na mawasiliano. Mfumuko wa bei umeendelea kubakia katika viwango vya chini, ukiwa katika wastani wa asilimia 3.3 mwezi Aprili 2021, na unatarajiwa kuendelea kuwa kati ya asilimia 3 na 5 katika kipindi kilichobaki cha mwaka wa fedha 2020/21. Hata hivyo, ongezeko la bei za mafuta kwenye soko la dunia linaweza kusababisha bei za mafuta nchini kupanda.
Urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje umeendelea kuimarika baada ya kupata athari za Corona kwenye biashara na uwekezaji. Mapato yatokanayo na mauzo ya dhahabu nje ya nchi yameongezeka hivyo kupunguza athari zilizotokea katika shughuli za utalii. Akiba ya fedha za kigeni imeedelea kuwa ya kutosha kukidhi mahitaji ya uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, na imeendelea kuwa sawia na makubaliano yaliyofikiwa katika nchi za EAC na SADC. Hali hii imewezesha kuendelea kuimarika kwa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni na kuwezesha kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri urari wa malipo. Kamati ya Sera ya Fedha imehimiza umuhimu wa kuongeza thamani ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na kutafuta masoko zaidi ili kudumisha ustahimilivu wa sekta ya nje.
Mikopo ya benki kwa sekta binafsi imeanza kuongezeka na kufikia ukuaji wa asilimia 4.8 kwa mwaka unaoishia mwezi Aprili 2021 kutoka asilimia 2.3 mwezi Machi 2021. Hali hii inatarajiwa kuendelea kuimarika katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2020/21, kutokana na mwendelezo wa sera wezeshi ya fedha na kuendelea kuimarika kwa shughuli za biashara na uwekezaji nchini na duniani. Aidha, sekta ya benki imeendelea kuwa imara, ikiwa na mtaji na ukwasi wa kutosha katika kuchangia ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi. Kamati imeridhika na juhudi za Serikali za kulipa malimbikizo ya wazabuni na marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani, hatua ambazo zitasaidia ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi na kuongeza mapato.
Kutokana na mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia, Kamati ya Sera ya Fedha imeridhia Benki Kuu kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi katika kipindi kilichosalia cha mwaka 2020/21. Hatua hii itasaidia ukuaji wa uchumi kupitia ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi. Mwisho, Kamati imeielekeza Benki Kuu kuendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi hapa nchini na duniani na kuchukua hatua stahiki za kisera pale itakapobidi.