Mkurugenzi wa Udhibiti, Ufuatiliaji na Tathmini wa NACTE, Dkt. Geofrey Oleke,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Kuhusu kufunguliwa kwa Dirisha la udahili wa wanafunzi katika ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa kozi zote zinazotolewa na vyuo vya elimu ya ufundi leo Mei 27,2021 jijini Dodoma.
………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Baraza la taifa la elimu ya ufundi hapa nchini NACTE tayari limefungua dirisha la udahili kwa wanafunzi katika ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa kozi zote zinazotolewa na vyuo vyote vilivyo chini ya Baraza hilo.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo Mei 27, 2021, Mkurugenzi wa Udhibiti, Ufuatiliaji na Tathmini wa NACTE, Dkt. Geofrey Oleke amebainisha kuwa vyuo vinaruhusiwa kupokea maombi ya udahili kuanzia leo hadi Agosti 14, mwaka 2021 katika awamu ya kwanza.
Dkt Oleke amebainisha kuwa vyuo vitachagua waombaji wenye sifa za kujiunga katika vyuo hivyo kati ya Agosti 15 hadi 20 mwaka huu, kisha Agosti 21 hadi Septemba 3, mwaka huu, majina ya waombaji waliochaguliwa yatawasilishwa katika Baraza hilo kwa ajili ya uhakiki.
Ameongeza kuwa majina ya wote waliochaguliwa na kuhakikiwa na NACTE yatatangazwa na vyuo husika Septemba 16, mwaka huu kwa ajili ya kuanza masomo Novemba Mosi, 2021.
Amesema kwa upande wa waombaji wote wanaoomba programu za afya kwenye vyuo vya serikali watatuma maombi yao moja kwa moja kupitia tovuti ya NACTE kuanzia siku ya leo hadi Agosti 14 majina ya watakochaguliwa yatatangazwa Agosti 22, mwaka huu.
Aidha Dkt Oleke amevitaka vyuo vyote vya mafunzo ya ufundi vitakavyopokea maombi ya wanafunzi kwa ngazi hizo kuzingatia taratibu na kanuni za udahili kama zilivyotolewa na baraza kwa mwaka wa masomo 2021/22, na watakao kiuka watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha NACTE imewataka wale waombaji wote wa elimu ya sekondari na vyuo wenye sifa za kujiunga na kozi hizo kufanya maombi yao kwa umakini ili kupata nafasi ya kujiunga na kozi wanazosipenda na walizotimiza vigezo vya kujiunga nazo kwa mwaka huo wa masomo.