********************************
Na Shamimu Nyaki,Mbeya
Waziri wa Habari, Itamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa amewaagiza Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kujituma kwa kasi, ari na weledi ambapo amesema atayezembea hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mhe.Bashungwa ameyasema hayo Mei 24, 2021 Jijini Mbeya wakati akifungua Kikao kazi cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali ambapo amesema kikao hicho kiwe chachu ya kuboresha utendaji pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya maafisa hao kwa mwaka 2021 ili kutekeleza kauli ya Baba wa Taifa Mwl. nyerere inayosema ” Kujikosoa ni Kujisahihisha”
“Nimeguswa na Kauli Mbiu ya kikao hiki kwa mwaka huu isemayo “Utoaji Taarifa kwa Umma ni Takwa la Kisheria Viongozi wa Umma na Maafisa Habari Tuwajibike, Hivyo
Wizara ninayoisimamia inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika kusimamia utoaji wa huduma za habari kwa umma, na hii ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016, na Sheria ya Haki ya Kupata Habari ya Mwaka 2016″ amesisitiza Mhe. Bashungwa.
Aidha Mhe.Bashungwa ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa Makatibu Wakuu wa Wizara yake na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha changamoto zote zinazowakabili maafisa hao ikiwemo kutoshirikishwa kwenye ziara za kutembelea miradi mbalimbali inayotokelezwa na Wizara au Taasisi, baadhi ya Maafisa Habari kuwekwa chini ya Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA) ambapo majukumu yake hayapewi kipaumbele pamoja na kutokuwa na bajeti, vifaa na bajeti ya Inteneti na Simu zinatatuliwa mara moja
Hata hivyo amewasisitiza Viongozi wa Wizara, Taasisi, Halmashauri za Wilaya, Manispaa Miji na Majiji kuhakisha wanatoa ushirikiano kwa maafisa habari ili watekeleze majukumu yao vizuri.
Kwa Upande wake Naibu Waziri Mhe.Pauline Gekul amesema Wizara yake inagusa watu wengi na ni Wizara inayozungumza, hivyo itaendelea kushirikiana kutatua changamoto za maafisa hao
“Natoa rai kwenu kufanya kazi kwa bidii, tuhabarishe umma mambo yote yanayotekelezwa na Serikali, tufanye kwa wakati na kuzingatia weledi na taaluma ya habari, pamoja na kuwa waadilifu” Mhe.Gekul.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Hassan Abbasi alitumia kikao hicho kushukuru maafisa hao kwa ushirikiano waliompatia wakati akiwa Mkurugenzi Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali na kuwasihi kuendelea kutekeleza majukumu yao vyema.
“Tuendelee kushirikiana katika Cheo kipya cha Katibu Mkuu katika Wizara hii ambayo ni Wizara muhimu katika kugusa umma kwa nyanja ya Burudani na Huzuni kutokana na Sekta zake”amesema Dkt. Abbasi.
Hata hivyo wakati kikao kinaendela Katibu Mkuu alipokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa maafisa hao
Akisoma ujumbe kwa Maafisa Habari na Uhusiano kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, Dkt.Abbasi amenukuu
“Naomba muendelee kuhimizana kuhusu umuhimu wa taarifa kwa Umma, yale yasiyo mazuri na yasiyo ya lazima kuwe na namna bora ya kutoa taarifa na msiache kusema mpaka wananchi waanze kulalamika ndiyo watoe taarifa”
Naye Katibu Mkuu TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe alisisitiza maafisa hao Maafisa Habari kutangaza miradi ya Serikali kwa umma.
Huku Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe.Juma Homera akitoa rai kwa Wakurugenzi kutenga bajeti kwa ajili ya Maafisa hao na kuwapatia vifaa mbalimbali wanavyohitaji katika kutekeleza majukumu yao.
Vilevile Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) Paschal Shelutete akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Maafisa hao amesema kikao hicho ni chachu ya kuendelea kuboresha utendaji wa maafisa hao.