Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, Emmanuel Chibago (wa pili kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya Miliki Chombo na NMB Jijini Dodoma inayolenga kuwakopesha vijana bodaboda na pikipiki za miguu mkitatu, Kushoto ni Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati – Nsolo Mlozi na mwisho kulia ni Mkuu wa Idara ya Biashara ya Kadi NMB – Philbert Casmir, Mkuu wa Idara ya Biashara- Alex Mgeni(mwenye fulana ya bluu) pamoja na Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Dodoma – Kenneth Chimoti.
Mameneja wa NMB matawi ya mjini Dodoma wakiashiria kuwa tayari kuelimisha vijana kuhusu mkopo wa bodaboda na pikipiki ya miguu mitatu ‘Miliki Chombo na NMB’ baada ya uzinduzi wa mpango huo Jijini Dodoma.
Waendesha bodaboda na pikipiki za miguu mitatu wakifurahia uzinduzi wa Miliki Chombo na NMB uliofanyika katika ukumbi wa Dear Mama – Jijini Dodoma.
***********************
Zaidi ya vijana 200 wa Jiji la Dodoma wanaojishughulisha na usafishaji wa abiria kwa bodaboda na pikipiki za miguu mitatu, jana walipatiwa mafunzo na Benki ya NMB ya jinsi gani wanaweza kujiongezea kipato na pia kuchangamkia fursa pale zinapopatikana.
NMB vile vile iliwapa elimu juu ya mikopo mbalimbali inayotolewa na benki hiyo ikiwemo ya bodaboda na pikipiki ya miguu mitatu kupitia mpango wao wa ‘Miliki Chombo na NMB’ – ambao kwa mwaka huu, imetenga Sh. bilioni 5 kwa ajili ya kuwakopesha kundi hilo.
Mpango huu wa Miliki Chombo na NMB umelenga kuwafikia vijana wengi nchini kote, kama njia ya kuwapa ajira vijana ambao bado hawajaingia katika mfumo wa ajira ili na wao waweze kupata kipato cha kujikimu kimaisha.
Akizungumza katika hafla ya uzunduzi wa mpango huu wa Miliki Chombo na NMB, Meneja wa NMB Kanda ya Kati – Nsolo Mlozi alisema mpango huo ni fursa tosha kwa vijana wenye nia ya kujiajiri, kwani pia masharti yake ni nafuu na kuwaasa vijana wengi kuchangamkia fursa hiyo. Lakini pia, aliwataka watembelee matawi ya NMB ili kupata ushauri zaidi ni namna gani wanaweza kuupata huo mkopo na wakutane na watalaam ili kujadili watakavyoweza kuendesha biashara hiyo kiurahisi.
Kwa upande wake Naibu Meya wa Jiji la Dodoma – Emmanuel Chibago aliiishukuru benki ya NMB kwa mpango huo, kwani ni mojawapo ya juhudi za kuiunga Serikali Mkono katika juhudi zake za kuongeza ajira kwa vijana.
Bwana Chibago aliwataka vijana watakao chukua mkopo huo kuwa waaminifu kwa NMB ili waweze kufikia malengo yao. Mpango huu Miliki Chombo na NMB umeshafika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.