*************************
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Damas Ndumbaro amesema kwa mujibu wa takwimu idadi ya tembo haijaongezeka nchini kama Watu wanavyodai.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Raha leo kilichopo kata ya Kalulu wilayani Tunduru katika Ruvuma wakati wa ziara ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi walioathiriwa na tembo.
Amefafanua kuwa licha ya matukio ya tembo kuvamia mashamba na kujeruhi baadhi ya wananchi kuongezeka lakini hayajachochewa na ongezeko la idadi ya tembo kama wengi wanavyodai bali ni idadi ya watu ndiyo iliyoongezeka
“Miaka ya 80 tulikuwa na Tembo takribani 134,000 na idadi ya Watanzania ilikuwa mil. 30 lakini hatukuwa na matatizo kama haya, Kwa sasa tuna tembo elfu 60 tu na idadi ya Watanzania imekuwa mil.60 , tujiulize akina nani wameongezeka, alihoji Dkt.Ndumbaro
Amesema hapo awali idadi ya tembo ilikuwa kubwa ila matukio kama hayo yalikuwa hayatokei kwa sababu maeneo mengi ya Hifadhi yalikuwa yalikuwa hayatumiwi na shughuli za kibinadamu kama ilivyo kwa sasa.
Amesema kwa sasa Wafugaji wamekuwa wakiingia ndani ya Hifadhi na makundi ya ng’ombe hali inayowalazimu tembo kutoka nje ya Hifadhi na kuanza kuvamia makazi ya wananchi kutokana na kushindwa kuchangamana na ng’ombe.
” Natoa agizo kwa Wafugaji walioingiza mifugo Hifadhini anzeni kuondoa wenyewe, Tukiikamata tutakutoza faini na tutaipiga mnada na ikiishindikana tutawapatia magereza kwa ajili chakula cha Wafungwa.
Aidha, Dkt.Ndumbaro ametaja sababu zingine za makundi ya tembo kuvamia makazi ya wananchi kuwa inatokana na baadhi ya watu kulima katika kingo za Hifadhi mazao pendwa kwa tembo, Hivyo tembo wamekuwa wakitoka njeya Hifadhi ili kuja kula mazao hayo.
Mbali na hiyo, Dkt.Ndumbaro amesema ongezeko la watu limechochea wananchi kuanza kulima na kujenga ndani ya shoroba na hivyo kuziba njia za tembo na hivyo tembo wanavyotaka kupita kwenye njia zake ni lazima walete adha katika maeneo hayo.
Kufuatia hali hiyo, Dkt.Ndumbaro ametoa wito kwa wananchi kuacha kuvamia shoroba na pia kuacha kulima kwenye kingo za Hifadhi.