Mkuu mpya wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akikabidhi Ofisi rasmi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Dk Binilith Mahenge (kulia) ambaye amehamishia Singida hafla iliyofanyika leo Mei 21,2021 jijini Dodoma.
Mkuu mpya wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekua RC wa Mkoa huo, Dk Binilith Mahenge (kulia) ambaye amehamishia Singida hafla iliyofanyika leo Mei 21,2021 jijini Dodoma.
Aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye amehamishiwa Singida, Dk Binilith Mahenge akizungumza wakati wa kumkabidhi ofisi Mkuu mpya wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka hafla iliyofanyika leo Mei 21,2021 jijini Dodoma.
Mkuu mpya wa Mkoa, Anthony Mtaka (mwenye shati jeupe) akiwa na aliyekua Mkuu wa Mkoa huo, Dk Binilith Mahenge ambaye amehamishia Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na Wakuu wa Wilaya za Dodoma baada ya Wakuu hao kukabidhiana ofisi hafla iliyofanyika leo Mei 21,2021 jijini Dodoma.
………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mkuu mpya wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Dkt Binilith Mahenge, huku akiwataka watumishi ndani ya Mkoa huo kila mmoja kutimiza majukumu yake kikamilifu na kwa weledi huku akibainisha kuwa elimu ni kipaumbe chake.
Akizungumza leo Mei 21,2021 jijini Dodoma mara baada ya kukabidhiwa ofisi Mtaka amesema kipaumbele chake kikubwa ni elimu ambapo ametaka kila mtu aondoke katika kikao hicho na agenda ya elimu kuhakikisha Mkoa unakuwa na ufaulu wa kuridhisha.
” Haiwezekani Shule ya Kwanza Simiyu inaingia 20 bora kitaifa halafu ya Kwanza hapa Dodoma inakua ya 103, ni lazima Wakurugenzi wa Halmashauri zote na Maafisa Elimu mtambue kipaumbele changu ni elimu, naamini katika Taifa lenye wasomi wengi katika kufikia mafanikio na ili Taifa lifanikiwe inabidi sisi huku chini tuanze.
Inatupasa kuandaa kizazi kipya cha Makao Makuu, kizazi chenye wasomi watakaoendana na hadhi ya Mkoa, wananchi watake wasitake watoto watasoma tu,” Amesema Mtaka.
Ameongeza kuwa “Kule Simiyu mwalimu akija ofisini kwangu na nikathibitisha kuwa mwalimu huyo amejibiwa vibaya na ofisi ya utumishi, mtumishi huyo anaondoka” amesema.
Ametoa wito kwa viongozi wote kuanzia Mkoani, Wilayani na Halmashauri kuwa wanyenyekevu na siyo kutumia nafasi na vyeo walivyonavyo kuumiza wengine.
” Mimi naamini katika ‘team work’ siyo jeshi la mtu mmoja hivyo kwa pamoja tukishirikiana tunaweza kuifanya Dodoma kuwa Mkoa wenye mafanikio makubwa kulingana na hadhi yake.
Tusifanye kazi kwa mihemko siyo mtu DC unanyanyua mabega kijana wa Chuo anakuletea wazo la kimaendeleo hata humsikilizi, unakuta mtu DC ana walinzi wanne huyo kiongozi atafikilia maendeleo kweli” amesema.
Kuhusu kilimo amemuomba Mkuu wa Mkoa mpya wa Singida, Dkt Binilith Mahenge kushirikiana katika mazao ya kimkakati kwa mikoa hiyo miwili ikiwemo alizeti ili kukomesha tatizo la uagizaji wa mafuta ya kula nje.
Amesema watahakikisha wanapambana kulifanya zao la alizeti kuwa zao la kibiashara ili kufanya lilimwe kwa wingi na kuondoa changamoto ya mafuta nchini ambayo imekua ikijitokeza.
Ametoa wito kwa kila kiongozi kwenye Mkoa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria za kazi huku akiwasihi kuwa wabunifu na wenye fikra chanya kulingana na mabadiliko ya kiteknolojia duniani.
Kutokana na Dodoma kuwa makao Makuu ya nchi amewataka viongozi kutoa kauli nzuri kwa wawekezaji wanapokuja kuwekeza katika Mkoa wa Dodoma, kwani uwekezaji unaweza kusisimua uchumi katika Mkoa wa Dodoma.
Awali aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ameshukuru kwa ushirikiano aliopewa na watumishi katika ngazi zote Mkoa wa Dodoma huku akitaka ushirikiano huo kuendelezwa kwa Mkuu mpya wa Mkoa.