Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (mbele, kulia) pamoja na viongozi mbalimbali kutoka wilayani Mbogwe mkoani Geita, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili mkoani Geita.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani pamoja na viongozi mbalimbali kutoka wilayani Mbogwe mkoani Geita, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili mkoani Geita.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani pamoja na viongozi mbalimbali kutoka wilayani Mbogwe mkoani Geita, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa umeme katika Kijiji cha Nyakasaluma wilayani Mbogwe. Kijiji hicho kimesambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa kwanza.
Miundombinu ya umeme katika Shule ya Msingi Nyakasaluma wilayani Mbogwe. Kijiji hicho kimesambaziwa nishati ya umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa kwanza
Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi (wa Tatu kutoka kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga na wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili uliofanyika katika Kijiji cha Mpakali wilayani Mbogwe, mkoani Geita.
…………………………………………………………………………..
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amezindua mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili mkoani Geita unaotarajiwa kusambaza umeme katika vijiji 117 ambavyo bado havina umeme mkoani humo.
Uzinduzi huo uliofanyika katika Kijiji cha Mpakali wilayani Mbogwe, mkoani Geita tarehe 17 Mei, 2021 ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Julius Kalolo, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.
“Katika Mkoa wa Geita, kuna vijiji 117 ambavyo bado havina umeme kati ya Vijiji takriban 474 na katika Wilaya ya Mbogwe, Vijiji 33 tu bado havina umeme kati ya Vijiji 87, hivyo leo tumeanza kuleta wakandarasi watakaoanza kazi ya kupeleka umeme katika vijiji ambavyo bado havina umeme kwa kuanzia hapa Mpakali.” Alisema Dkt.Kalemani
Alieleza kuwa, mradi huo utatekelezwa katika kipindi cha miezi 18 na Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 75.6 kwa ajili ya shughuli hizo za usambazaji umeme vijijini mkoani Geita.
Aidha, ili miradi ya umeme vijijini iweze kuwa na tija, Dkt.Kalemani aliwahimiza wananchi kote nchini kuhakikisha kuwa wanaunganisha umeme mara unapofika kwenye maeneo yao kwani Serikali inatumia fedha nyingi kufikisha miundombinu ya umeme sehemu mbalimbali nchini.
Vilevile alieleza kuwa, bei ya umeme vijijini ni shilingi 27,000 tu na kwamba Taasisi za umma kama vile Shule, Zahanati, Misikiti, na Makanisa zipewe kipaumbele cha kuunganishiwa umeme mara miundombinu ya umeme inapofika katika maeneo husika.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati, alisema kuwa mradi wa usambazaji umeme katika vitongoji ambavyo bado havina nishati ya umeme nchini utaanza mwezi Julai mwaka huu na utatekelezwa ndani ya miezi 12.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga alisisitiza masuala mbalimbali ikiwemo wananchi kuchangamkia fursa za kuunganisha umeme kwa shilingi 27,000 tu na nishati ya umeme kufika kwenye Taasisi za umma kama vile Zahanati na Shule ili kuweza kuleta manufaa.
Akiwa wilayani Mbogwe, mkoani Geita, Waziri wa Nishati pia aliwasha umeme katika ;Kijiji cha Nyakasaluma ambacho kimesambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza.
Kuhusu kazi ya usambazaji umeme vijijini nchini, alisema kuwa mpaka sasa ni vijiji 1,956 tu ambavyo havijasambaziwa umeme kati ya vijiji 12,268.