Afisa Mipango Miji ofisi ya Ardhi Mkoa Venance Mndaza akitoa elimu ya mipango miji katika kijiji cha Ilemba muda mfupi baada ya kijiji hicho kupandishwa hadhi na kuwa mji mdogo.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Rukwa Swagile Msananga akitoa ufafanuzi baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya migogoro ya iliyopo vijijini.
*******************************
Kutokana na kasi ya ukuaji wa vijiji inayochangiwa na maendeleo ya wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo, timu ya ofisi ya Ardhi Mkoa wa Rukwa imekutana na wananchi wa vijiji vya Kilyamatundu, Ilemba, Muze na Mtowisa na kuwatangazia wananchi hao kuwa vijiji hivyo vimepandishwa hadhi na kuwa miji midogo.
Pamoja na kutoa taarifa hiyo, timu hiyo imeendelea kukutana na wananchi katika mikutano ya vijiji na kutoa elimu ya sheria za ardhi na urasimishaji wa makazi katika maeneo yaliyoiva kimipango miji ili waweze kuhama kutoka umiliki wa ardhi kimila na hatimae kuwa chini ya serikali kuu na jambo litakalotimiza azma ya serikali katika kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini.
Hatua hiyo ya kuvipandisha hadhi vijiji hivyo vilivyopo katika bonde la ziwa rukwa, wilayani Sumbawanga, Mkoani Rukwa imetokana na vijiji hivyo kufikia vigezo vya kuwa miji midogo, vigezo ambavyo ni pamoja na kuwa na mzunguko mkubwa wa fedha na uchumi na wingi wa wakazi na makazi.
Akizungumza baada ya mkutano na wananchi katika Kijiji cha Muze Kamishna Msadizi wa Ardhi Mkoa wa Rukwa Swagile Msananga alisema kuwa endapo vijiji hivyo vinavyokuwa kwa kasi havitawahiwa kupangwa na kupimwa itapelekea kuwa na makazi mengi holela jambo ambalo serikali isingependa kuona na kuongeza kuwa wataendelea na zoezi hilo katika maeneo na vijiji vingine vya mkoa wa Rukwa.
“Baada ya zoezi la urasimishaji kufanyika, kwa maana ya kwamba makazi yatakuwa yamepangwa na kupimwa, wananchi tunatarajia kuwapa hatimiliki, kila mwananchi atamiliki kipande chake cha ardhi kwa hati miliki ambayo itatolewa na serikali, tunataraji kwamba baada ya kupata hatimiliki wananchi wataweza kuwa na fursa ya kutumia hatimiliki katika kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha au kutumika kama dhamana, mahakamani mara nyingine huitaji dhamana ya mali isiyohamishika,” Alisema.
Msananga aliongeza kuwa pia zoezi hilo la urasimishaji linatarajiwa kupunguza migogoro kwa kiasi kikubwa ama kuimaliza kabisa hali ambayo itawapelekea watu kujikita katika shughuli za kimaendeleo na kujiendeleza Zaidi kiuchumi.
Venance Mndaza ni afisa mipango miji ofisi ya ardhi mkoa ambae nae kwa upande wake aliongeza kuwa pamoja na zoezi la urasimishaji pia serikali imelenga kuongeza wigo wa makusanyo ya maduhuli ya serikali kutokana na tozo mbalimbali za sheria ya ardhi
“Kumbuka kwamba eneo hili likishapangwa tayari tutaweza kukusanya mapato, kutoka vibali vya ujenzi, tozo za umilikishaji wa ardhi, tozo za ubadilishaji wa miji, kwahiyo hayo yote ni mapato ambayo tunategemea kwa siku za usoni yataweza kuongeza makusanyo katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na katika wizara ya ardhi kwa maana ya serikali yetu kwa ujumla, Alisema.
Mmoja wa Watendaji wa vijiji hivyo, mtendaji wa Kijiji cha Ilemba Edson Chikondo alitaja baadhi ya faida zitakazopatikana kutokana na kupandishwa hadhi kwa Kijiji hicho kuwa ni Pamoja na kuimarika kwa miundombinu iliyopo Kijiji hapo na kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara katika mitaa na sio kutegemea barabara kuu.
Katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika, timu hiyo ya ofisi ya ardhi imeunda kamati ya urasimishaji iliyowajumuisha wananchi nane waliochaguliwa na wakazi wa Kijiji husika katika kila Kijiji Pamoja na kuanza taratibu za kufungua akaunti ya benki ili kila kaya kuweza kuchangia shilingi 50,000/=, fedha itakayosaidia kukamilisha zoezi la urasimishaji katika vijiji hivyo huku matumizi ya fedha hizo yakiamuliwa na mkutano wa Kijiji husika.