***************************************
Na Emmanuel J. Shilatu
Waliosema “Wembe ni ule ule” hawakukosea tena huu wa sasa ni mkali zaidi pande zote. Hayo yamejidhirisha kwenye uchaguzi mdogo wa marudio wa majimbo mawili ya Muhambwe na Buhigwe, na kata 5 ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kwa kishindo kwa asilimia 100.
Ushindi huu wa CCM unakuja kipindi ambacho CCM ina Mwenyekiti CCM Taifa mpya ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na sekretarieti mpya Taifa ambao hawajafikisha hata mwezi mmoja lakini wameweza kujipanga vyema na kuibuka na ushindi wa kimbunga.
Ushindi wa CCM unatokana na kujipanga vyema kuanzia wagombea, sera, kunadi ilani ya uchaguzi, mtandao mpana ulionao kuanzia ngazi ya shina mpaka Taifa pamoja uimara wa timu kampeni ya ushindi ambao kwa nyakati zote wamefanya siasa safi, za kistaarabu. Hakika CCM mpya ya Samia imeonyesha ukomavu mkubwa ndani ya muda mfupi.
Si viongozi wa vyama vya upinzani, si Wananchi, si waangalizi wa uchaguzi kote ambapo pamefanyika uchaguzi wote wamekiri uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Pongezi za kipekee zimfikie Katibu Itikadi na uenezi CCM Taifa Ndugu Shaka Hamdu Shaka kwa kupanga vyema safu za kampeni kote uchaguzi ulipofanyika ndani ya muda mfupi na kuibuka na kimbunga cha ushindi.
Shaka ameonyesha kuamini katika umoja, ushirikiano na mshikamano ambapo tumeona Watu mbalimbali wakipata fursa ya kunadi na kupiga kampeni tofauti na awali. Ule msemo wa “Umoja ni ushindi” umedhihirishwa kwa vitendo kupitia kwa Mwenezi Shaka Hamdu Shaka.
Ushindi huu wa CCM una maana kubwa sana kwani umeonyesha imani kubwa walionayo Watanzania kwa Rais Samia; Umeonyesha imani kubwa kwa CCM kuwa ndio chama pekee tumaini na tegemeo la Watanzania wote katika kuwakomboa na kuwaletea maendeleo. Nikiwa kama Mtanzania Mzalendo wa nchi yangu, najivunia heshima hii kubwa na ya kipekee ambayo Watanzania wameonyesha kwa Rais Samia, wameonyesha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Narudia tena kuipongeza CCM kwa ushindi mnono wa 100% kwenye uchaguzi mdogo wa marudio. Hakika hii ndio CCM mpya iliyoanza kwa mwendo kasi na matumaini makubwa kwa Watanzania wote.
*Shilatu, E.J*