………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
SHEIKH Mkuu wa mkoa wa Pwani, Hamis Mtupa ,amekemea vitendo vya ubakaji hususan kwa watoto ,vitendo vinavyodaiwa kushamiri katika baadhi ya maeneo ,na kuiomba jamii kushirikiana kupiga vita vitendo hivyo.
Aidha ameitaka jamii kusimamia maadili na kudumisha tamaduni za kitanzania ,bila kuendekeza masuala ya utandawazi.
Alitoa rai hiyo katika sikukuu ya Eid pili na baraza la eid lililofanyika Misugusugu Kibaha Mjini .
Mtupa alieleza, masuala ya ubakaji ni masuala ya kipolisi na ni mamlaka inayopaswa kuzungumzia zaidi hali hiyo ,lakini wameagizwa na vitabu vya dini kukemea maovu ikiwemo ubakaji na uhalifu mbalimbali.
Alibainisha kwamba, hivi karibuni alihudhuria hafla ambayo Jeshi la polisi Pwani lilithibitisha vitendo hivi kuongezeka ukilinganisha na matukio ya ajali ambayo kwasasa yanapungua mkoani hapo.
“Nililibeba hili ,kwakuwa limegusa jamii, na vitabu vya dini vinaruhusu kukemea nimepanga kila ninaposimama kuongea basi nitakemea hili ,na nawaomba viongozi wengine tusiliache hili linakua kwani watoto wanazidi kufanyiwa ukatili huu” alisema Mtupa.
Mtupa aliwataka ,viongozi wa serikali za mitaa kusimamia matukio hayo yasitokee na endapo yakitokea wasibebane wala kufumbia macho .
“Suala hili linashirikishwa na masuala ya ushirikina ,ila mimi nakataa ,msifuate waganga na kupotoshwa ,baba na mama kemeeni hili ,hakuna utajiri unaokuja kwa kubaka kichanga,mtoto wako !!!hili linasababisha na wale wenye maambukizi ya VVU kumpa mtoto Ukimwi asiye na hatia.” alisisitiza Mtupa.
Kwa upande wake ,mgeni maalum mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema ,ameshiriki kuandaa baraza la eid ikiwa ni kawaida yake kila mwaka .
Alisema ataendelea kushirikiana na dini zote kutatua shughuli mbalimbali bila kujali itikadi za kidini .
Koka pia ,aliwaomba wananchi kuendelea kufuata taratibu za kiafya kwa kunawa mikono, kuepuka mikusanyiko ili kujihadhari la gonjwa la corona.
Awali mjumbe wa baraza la masheikh Pwani,Athuman Mtasha alisema amani iendelee kudumishwa .
Aliwaasa waumini wa kiislamu ,kuwa watii kwa viongozi mbalimbali ,kuwa na nidhamu na kufuata misingi ya dini hiyo.