Mkurugenzi Msaidizi Utunzaji wa Vyanzo vya Maji, Rosemary Rwebugisa akizungumza wakati wa kufunga warsha ya Usalama wa Mabwawa. Kulia ni Mhandisi Mkuu kutoka Wizara ya Maji, Abdallah Mataka na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Mabwawa, Domina Msonge.
Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Mabwawa, Domina Msonge akizungumza wakati wa warsha ya wadau kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa.
Baadhi ya washiriki wa warsha kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kutoka kwa wataalam (hawapo pichani).
**********************
WADAU wa mabwawa wamesisitizwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo na kuhakikisha mabwawa yanasajiliwa kwenye Mamlaka husika ili yatambulike kisheria kwa lengo la kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa jamii na mazingira kwa ujumla.
Wito huo umetolewa hivi karibuni Jijini Mwanza na Mkurugenzi Msaidizi Utunzaji wa Vyanzo vya Maji kutoka Wizara ya Maji, Rosemary Rwebugisa wakati wa kufunga warsha ya wadau kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa.
“Zingatieni Miongozo ya Usalama wa Mabwawa, tunahitaji uwepo wa mabwawa yenye manufaa na ambayo ni salama kwa viumbe hai na mazingira na si vinginevyo,” alielekeza Rwebugisa.
Rwebugisa alisisitiza umuhimu wa kutumia Watalam wa Mabwawa waliosajiliwa kuanzia hatua za awali za usanifu hadi hatua ya usimamizi wakati tayari yameanza kazi ili kuepukana na changamoto zinazoweza kusababisha madhara.
Alisema baaadhi ya mabwawa hukutana na changamoto kadhaa huku mengine yakishindwa kukidhi matakwa ya matumizi yaliyokusudiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kutoshirikisha wataalam.
“Kabla hamjaanza kuchimba ama kujenga mabwawa hakikisheni mnashirikisha wataalam ili wajiridhishe kulingana na utaalam wao kama bwawa linalotarajiwa kujengwa mahali hapo linastahili na pia namna gani lijengwe ili kuepukana na changamoto zinazozuilika,” alisisitiza Rwebugisa.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazoweza kujitokeza endapo bwawa litajengwa bila ushauri wa kitaalam ni pamoja na kuvuja, jambo ambalo alisisitiza kuwa ni hatari kwa afya na maisha ya viumbe wanaozunguka eneo husika.
Alisema jamii pia inapaswa kuelimishwa na kutambua umuhimu wa mabwawa hasa ikizingatiwa kwamba mabwawa yanazo faida lukuki ambazo baadhi yake alizitaja kuwa utunzaji wa mazingira kwa kuhifadhi taka hatarishi lakini pia ni chanzo cha mapato kutegemeana na aina ya bwawa.
“Mabwawa yana faida nyingi sana, ni muhimu jamii ikaelimishwa juu ya faida hizo lakini pia namna ya kuyalinda na kuyatunza ili kuepusha madhara,” alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu warsha, Rwebugisa alisema imejikita kujadili Miongozo ya Usalama wa Mabwawa na kwamba wadau walioshiriki wajitahidi kufuata miongozo walioijadili.
Alielekeza washiriki kuhakikisha wanaendelea kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha usalama wa mabwawa na kuendeleza mawasiliano ya karibu na ya kila mara na Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wake.
“Mapendekezo yenu tumeyachukua kwa maboresho kwani miongozo iliyopo sio misahafu hivyo tutakuwa tunaboresha kila tunapoona kwa pamoja umuhimu wa kufanya hivyo,” alisema.
Warsha hiyo imeshirikisha Viongozi kutoka Wizara ya Maji, Wawakilishi kutoka Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wa mabwawa, Wataalam wa Mabwawa (APPs), Wizara na Taasisi zinazomiliki mabwawa, makampuni yanayomiliki mabwawa, Ofisi za Mabonde na Wawezeshaji wa mafunzo.