Na Baltazar Mashaka, Mwanza
KAMATI ya Mpito ya Taasisi ya Msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza, inatajwa kuhusika kwenye ubadhirifu wa fedha za kodi ya pango,mali ya msikiti huo.Uchunguzi wa gazeti hili umebaini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kuitia vyanzo na taarifa mbalimbali umebaini baadhi ya viongozi wa kamati hiyo wanahusika kufanya ubadhirifu wa fedha za kodi ya upangaji kwa maslahi yao kutoka kwenye kiwanja Namba 50 Kitalu Q kilichopo kwenye maungio ya mitaa ya Uhuru na Mission wilayani Nyamagana.
Mbali na kiwanja hicho pia wanadaiwa kufanya ubadhirifu kwenye miradi mingine mali ya msikiti huo uliopo katikati ya Jiji la Mwanza.
Habari kutoka vyanzo vyetu vya kuaminika ambazo hazijathibika zinaeleza kuwa Kamati ya Mpito ya Msikiti wa Ijumaa inatumia ulaghai kwa wapangaji kuwa akaunti za msikiti zilizopo kwenye benki za KCB na Amana zimefungwa na hivyo kukusanya fedha taslimu ili kuhalalisha ukwapuaji wa wajumbe wa kamati hiyo.
Katibu wa Bodi ya Wadhamini inayodaiwa kuvunjwa na RITA, Sheikh Abdallah Amin,alisema kamati ya mpito inakusanya fedha taslimu kwa wapangaji badala ya kulipwa kwenye akaunti,kinyume cha maelekezo ya RITA kwa kisingizio cha akaunti za msikiti kufungwa.
“Suala la kamati ya mpito kuchukua fedha taslimu kwa wapangaji wakati wanatakiwa (wapangaji) wazipeleke benki za KCB na Amana,tumelalamika RITA sana,stakabadhi zinaandikwa fedha kidogo tofauti na zilizokusanywa,huo ni utakatishaji ili kuepuka mali za waislamu kunufaicha wachache tunaomba serikali ifanye ukaguzi wa fedha,”alisema Sheikh Abdallah.
Kwa mujibu wa nyaraka (nakala tunayo),viongozi hao wanadaiwa kuchukua kodi ya sh. milioni 2 za kodi ya pango ya mwaka mmoja kwa mmoja wapangaji kwenye kiwanja hicho ambaye amejenga miundombinu ya jengo la biashara (mgahawa)lakini kwenye stakabadhi ya malipo akaandikiwa sh. 700,000.
Mpangaji huyo Daniel Semuguruka, Machi 29,mwaka huu, aliruhusiwa na Kamati ya Mpito kujenga na kufungua biashara ya mgahawa eneo tajwa Machi 29, mwaka huu ambapo alilipa kodi ya pango sh. milioni 2 kwa mwaka mmoja, kuanzia Aprili 1, 2021 hadi Machi 31, 2022.
Alisema baada ya upande wa pili wa mgororo kuzuia kujenga miundombinu ya biashara alilazimika kulipa sh. 500,000 za kibali cha ujenzi wa banda la muda la biashara ya Baba Lishe kwenye kiwanja namba 50 Kitalu Q, ambazo aliwakabidhi baadhi ya viongozi hao bila maandishi, pia alilipa sh.450,000 kati ya zaidi ya sh.700,000 za deni la Ankara ya matumizi ya maji.
Kuhusu stakabadhi ya malipo kuandikwa sh. 700,000 aanadai kutishwa na viongozi hao wa kamati ya mpito kuwa yeye ni baba lishe hivyo ikiandikwa kodi ya sh. milioni 2 TRA watambana na kumtoza kodi kubwa.
“Fedha hizo niliwakabidhi msikitini,ukiwa kanisani au msikitini unajua hakuna ujanja ujanja wala ufisadi, hivyo sikuwa na hofu kuwa nimeingizwa mkenge ambapo mmoja alijitambulisha ni katibu wa kamati ya mpito,”alisema Semuguruka.
Katibu wa Kamati ya Mpito Idrisa Haesh, alipoulizwa kwa simu kuhusu suala la malipo ya kodi ya wapangaji kwenye kiwanja Namba 50 kinachomilikiwa na Msikiti wa Ijumaa,kuandikwa tofauti kwenye stakabadhi na mvutano uliopo kati ya kamati hiyo na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Msikiti huo alikuwa mbogo.
“Kamati ya Mpito ilishaundwa lakini wapo watu wanadai wao ni viongozi ndio wanaoleta matatizo na kuwataja kuwa ni Abdallah Amin na Sherally (Hussein) pamoja na Khalid Abdallah, bado wanahisi wana nafasi,”alisema.
Akijibu hoja ya Sheikh Hamza kuwa yeye Sheikh Abdallah Amini ndiye chanzo cha mgogoro alisema unakuzwa na RITA kwa maslahi yao na mtu mmoja aliyejificha kwenye kivuli cha shule ya Thaqafa,kama bodi ilivunjwa yeye Sheikh Hamza Mansour anabaki kama nani ilhali naye alikuwa kwenye bodi.Je,taratibu za kuivunja bodi zilifuatwa na aliyempa Uimamu anahusika vipi na Msikiti wa Ijumaa ?
Aidha Sheikh Abdallah alikanusha madai ya Idrisa Haesh,kuwa ameshitakiwa mahakamani si kweli,wanaoshitakiwa na Shule ya Thaqaafa ni Bodi ya Msikiti wa Ijumaa (inayodaiwa kuvunjwa), Abdallah Amin na Sherally Hussein hivyo suala la kukusanya kodi ya pango kwa wapangaji haliko mahakamani.