……………………………………………………………………………….
Mrajis wa vyama vya Ushirika Nchini Dkt Benson Ndiege amewataka Viongozi,wanachama wa Ushirika na wakulima kuja kujifunza soko la mfumo wa stakabadhi ghalani mkoani Ruvuma kwa sababu Mkoa umefanikiwa katika kusimamia na kuendesha soko hilo.
Dkt Ndiege ametoa kauli hiyo wakati akishuhudia ufunguzi wa soko la pili la mnada wa kitaifa wa mazao yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma hivi karibuni.
Dkt Ndiege amesema mkoa wa Ruvuma umefanikiwa katika kuelimisha wakulima na kuwaunganisha pamoja katika soko la mfumo wa stakabadhi ghalani,hivyo amewataka Viongozi,wanachama wa Ushirika na wakulima kufika Ruvuma kujifunza juu ya mfumo huo.
“Nyie Songea au Ruvuma ni mfano mzuri kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani nawapongeza”,amesema Dkt Ndiege.
Amesema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mfumo shirikishi kwa wakulima na wafanyabiashara ambao unatoa fursa kwa wakulima kukusanya na kuuza mazao yao kwa pamoja na kutatua changamoto za ukosefu wa soko la uhakika vilevile humpunguzia mnunuzi gharama za ufuatiliaji na uhakika wa kupata mazao yenye ubora.
Amewataka wafanyabiashara kujali maslahi ya wakulima kwa kununua mazao hayo kwa bei ambayo hai mkatishi tamaa mkulima katika kuendelea kuzalisha zao hilo ambalo uzalishaji wake ni mgumu ukilinganisha na mazao mengine.
Kwa upande wake Afisa shughuli wa chama kikuu cha Ushirika cha SONAMCU Zamakanaly Komba amesema katika soko la mfumo wa stakabadhi ghalani wakulima ndiyo mtaji katika kuendesha soko hilo na wanamamlaka ya kukubali au kukata kuuza mazao yao endapo bei inyotajwa kutokuwa na maslahi kwao.
Komba amesema kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021 katika soko la kwanza la mnada jumla ya tani 164 zilikusanywa toka kwa wakulima kupita Vyama vya Msingi vya Ushirika ambapo wakulima walikata kuuza kutokana bei kutowaridhisha ya shilingi 2210 kwa kilomoja.
Kwa upande wa wakulima wamedai bei hiyo ni ndogo wametaka wastani wa bei ianze na shilingi 3000 hadi shilingi 2500 kwa kilomoja ambayo inamaslahi kwao kulinga na gharama za uzalishaji.
Naye afisa kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Hellen Shemzigwa amesema kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 Halmashauri inatarajia kuuza taani 2600 za ufuta.
Mfumo wa stakabadhi ghalani katika mkoa wa Ruvuma umewaingizia wakulima zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 28 kwa mazao ya ufuta,soya,na mbaazi katika msimu wa masoko wa mwaka 2020/2021.