Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahan akishiriki kupakia matofali kuzipeleka eneo la ujenzi wa nyumba tano za watumishi.wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahan (wa tatu walio kaa kutoka kushoto) akiwa na Vijana wa Kikundi cha Jitume Vijana Ikungi.baada ya kutembelea mradi wa ufyatuaji matofali wilayani humo jana.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KAIMU Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani ameipongeza Halmshauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kuwawezesha vijana kiuchumi.
Ndahani alitoa pongezi hizo jana alipotembelea mradi wa vijana wa ufyatuaji wa matofali wa Jitume Vijana Ikungi.
Ndahani alisema Wilaya ya Ikungi imekuwa ya kuigwa mfano kwa utoaji wa mikopo na kuwapatia tenda vijana ndani ya halmashauri hiyo.
” Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imewapatia tenda vijana wa Vikundi vya Jitume na Puma Youth Group kuuuza matofali katika mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba tano za watumishi.” alisema Ndahani.
Aidha Ndahani amewaomba wakurugenzi na Madiwani kuhakisha wanatimiza sheria ya utoaji wa mikopo kwa makundi maalumu kwa mujibu wa Sheria ya fedha za Serikali za mitaa Sura 290 kifungu 37, pamoja na kuwapatia tenda vijana.
Alisema yakifanyika hayo watakuwa na lengo dhabiti la kuwakwamua vijana na umaskini katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine Ndahani amewataka vijana kuhakikisha wanarudisha kwa wakati mikopo wanayokopeshwa ili kuwapa fursa vijana wengine kukopa.
Ndahani aliwaambia vijana hao kuwa Serikali ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inawapenda na kuwajali na kuwa itaendelea kuwawezesha kuwapa mikopo ya masharti na riba nafuu kupitia Serikali za mitaa, Ofisi ya Waziri Mkuu na Benki ya maendeleo ya kilimo (TADB).
” Ni wajibu wetu vijana kuchapa kazi kwa nguvu na weledi ili kuinua uchumi wetu binafsi na Taifa kwa ujumla.” alisema.
Alizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Afisa Maendeleo wa wilaya hiyo Kaweso Gadiel , alisema ofisi yao imeamua kufanya hivyo ili kuwainua vijana wa Ikungi kwa lengo la kufikia adhima ya kuondokana na umaskini hivyo wamepatiwa mikopo na tenda hiyo kutokana na vikundi hivyo kutengeneza natofali yenye ubora wa hali ya juu.
Esther Isula akizungumza kwa niaba ya vijana hao wa Kikundi cha Jitume Vijana Ikungi alisema Halmshauri ya Ikungi imewapatia mkopo wa Sh.milioni 16,622,000 na tayari wameresha milioni 9,222,0000.
Vijana hao wameishukuru Halmshauri ya Wilaya ya Ikungi chini ya Mkurugenzi Justice Kijazi kwa kuwapatia mkopo na tenda ya kuuuza matofali katika ujenzi wa nyumba hizo tano za watumishi