Askofu wa Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria Mwanza, Askofu Andrew Gule akimsimika Askofu mteule Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, kuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Lushoto Mkoani Tanga, Mei 9, 2021
Askofu wa Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria Mwanza, Askofu Andrew Gule akimvisha kofia Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kama alama ya kazi ya ukuhani unavyokabidhiwa katika kanisa la Mungu, wakati wa tukio la kuwekwa wakfu na kusimikwa kazini kwa Askofu Dkt. Msafiri, Lushoto Mkoani Tanga, Mei 9, 2021.
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini kati, Askofu Dkt. Solomoni Massangwa akimkabidhi fimbo Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kama ishara ya Mchungaji mwema aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kondoo, wakati wa tukio la kuwekwa wakfu na kusimikwa kazini kwa Askofu huyo, Lushoto Mkoani Tanga, Mei 9, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu baada ya kusimikwa kuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, kushoto ni mke wa Askofu huyo Marry Msafiri Mbilu, Lushoto Mkoani Tanga, Mei 9, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), baada ya tukio la kusimikwa kwa Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Lushoto Mkoani Tanga, Mei 9, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini katika mahubiri yao waweke msisitizo katika masuala ya kuwekeza kwa vijana ikiwa ni pamoja na kukemea vitendo vyote hatarishi visivyozingatia maadili ya Mtanzania.
“Tusisahau pia kwamba ukimwi bado upo. Aidha, vijana wengi wapo katika hatari ya kupata maambukizi. Kwa Msingi huo, tumieni nafasi yenu katika jamii kutoa ushauri nasaha na hatimaye kupunguza kasi ya maambukizi kwa vijana”.
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Mei 9, 2021) katika ibada ya kusimikwa kwa Askofu Dkt. Msafiri Mbilu, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Lushoto. Waziri Mkuu ameshiriki ibada hiyo kwa niaba ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi na majukumu makubwa ya Viongozi wa Kanisa ambayo ni pamoja na kuwaongoza watu kiroho na kuwapa mafundisho, ushauri na kuwajenga kiimani.
Mheshimiwa Majaliwa amesema “Hubirini masuala ya vijana kwani kauli yenu inapokelewa vizuri kwenye jamii na watu wa rika zote. Endeleeni kuwasaidia watu katika shida mbalimbali hususan wale wenye uhitaji kama yatima na wajane”.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi hao waendelee kutoa mafundisho yenye kuhimiza wananchi wadumishe amani na utulivu nchini kwa manufaa ya vizazi vya sasa na ya vizazi vijavyo.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inatambua kwamba maendeleo ya nchi hayawezi kwenda bila ya ushirikiano na sekta binafsi na kwa kuzingatia hayo, imekuwa ikishirikiana na Sekta binafsi zikiwemo Taasisi za dini katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa.
Amesema Serikali imekuwa ikishirikiana na Dayosisi hiyo katika utoaji wa huduma za afya kwenye hospitali zake zilizopo Bumbuli, Kilindi na Lutindi Mental Hospital kwa kutoa dawa pamoja na kuleta madaktari na watumishi ndani ya hospitali hizo ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma stahiki na kwa wakati.
“Nitumie nafasi hii tena kuwahakikishia kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano huu kwa manufaa ya Watanzania wote. Nitoe Rai kwa viongozi mnaowekwa wakfu leo kuwa viongozi wa Dayosisi hii ya Kaskazini Mashariki muendelea kuhubiri amani, upendo na mshikamano kwa wana Dayosisi na kwa Watanzania wote kwa ujumla”.
Hizo ndizo Tunu alizotuachia Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambazo zilitunzwa na kuheshimiwa na viongozi wote waliopita, na zitaendelea kutunzwa katika awamu hii ya uongozi. Vilevile msichoke kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali kwa maendeleo ya jamii ya Watanzania”.
Kwa upande wake, Askofu Dkt. Mbilu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kushiriki katika ibada na amemuhakikishia kwamba Dayosisi yao itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo pamoja na kudumisha amani