Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel.
Mlezi wa TAMUFO, Frank Richard.
Na Dotto Mwaibale
UMOJA wa Wanamuziki Tanzania ( TAMUFO) umempongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa kwa kusikia kilio chao kwa kuwatoa hofu Wasanii kuhusu suala la ugawaji wa Mirabaha.
Hatua hiyo ya Bashungwa imekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya TAMUFO kuliomba Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuhakikisha linashirikisha wadau wa muziki kabla ya kutoa maamuzi ya kuwabana wasanii.
Ombi hilo lilitolewa na Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel jijini Arusha juzi baada ya kutokea malalamiko ya wanamuziki kulalamikia kitendo cha Basata kuweka utaratibu wa kuwataka wanamuziki nyimbo zao zikaguliwe baada ya kurekodi kwa sababu za kimaadili.
Joel alisema jambo hilo lilikuwa linawaumiza wanamuziki wa Tanzania ambao wanahangaika sana kuwezakumudu gharama za kurekodi kazi zao.
Katibu mkuu huyo wa TAMUFO Stella Joel alisema wanamuziki wengi hawana kipato cha kutosha na kurudia rudia katika kurekodi kazi zao na bado hawajaweza kufaidika nazo.
Akizungumza jana jijini Dodoma katika kikao chake na Viongozi wa Vyama na Mashirikisho ya Muziki na Filamu nchini kilicholenga kuzungumzia Kanuni ya 26 ya BASATA inayohusu uhakiki wa kazi za Muziki na Filamu kabla ya kuingia sokoni au kusambazwa, Bashungwa aliwatoa hofu wasanii kuhusu suala la ugawaji wa Mirabaha kwa kuelezea kuwa Serikali imeandaa mifumo ya kidijitali ambayo itarahisisha ukusanyaji wa mirabaha hiyo na kuongeza gawio.
“COSOTA imekuwa na changamoto ya ukusanyaji wa mirabaha kutokana na uhaba wa watumishi hivyo kwa kupitia mfumo mpya wa kidijitali utakao anzishwa hivi karibuni utarahisisha ukusanyaji wa mirabaha hiyo, Serikali inataka kutoa gawio la pesa nyingi kwa wasanii na siyo fedha kidogo hivyo tunawaomba mvumilie kidogo kuanzia mwaka mpya wa fedha mambo yatakuwa mazuri.” alisema Bashungwa.
Akiendelea kuzungumza katika kikao hicho Bashungwa alitoa maelezo mahususi kwa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) akiwataka kusitisha utekelezaji wa Kanuni ya 26 inayotaka kazi zote za Muziki kukaguliwa nao kabla ya kusambazwa.
Aidha, Bashungwa alisisitiza kuwa maelekezo hayo ya kusikitishwa kwa matumizi ya kanuni hiyo ni kwa upande wa Muziki pekee ila kwa upande wa Filamu itaendelea kutumika kama kawaida.
Pamoja na hayo Bashungwa alitoa maelekezo ya haraka kwa BASATA kwa kuwataka kuanzisha mchakato wa kurekebisha kanuni hiyo kwa kuwashirikisha wadau hao wa vyama na mashirikisho ili kuweza kupata Kanuni mpya isiyodumaza tasnia ya Muziki lakini izingatie maadili ya Taifa.
Halikadhalika Waziri huyo ameelekeza BASATA kwa kushirikiana na wadau kuandaa mwongozo utakao kuwa kukitoa dira njema ya uendeshaji na ukuzaji wa tasnia ya Muziki.
Naye mmoja wa wasanii hao Soggy Doggy alimshukuru Bashungwa kwa maamuzi aliyoyafanya na kumpongeza na kuahidi kuendelea kushirikiana na wasanii wa Muziki katika kukuza na kuiendeleza tasnia ya muziki nchini.