**************
NA MWAMVUA MWINYI,MKURANGA
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali amewashukia baadhi ya watendaji wa chini ambao wamekuwa wakihujumu ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji huku akielekeza mtendaji atakaebainika kushiriki katika hujuma hizo awajibishwe.
Amewaagiza wakuu wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani ,kuwashukia wazima wazima watendaji wa aina hiyo wasiwaonee huruma .
Akizungumza katika makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru Mwandege, Mkuranga mkoani Pwani ,ukitokea jijini Dar es salaam ,Ali alisema haiwezekani serikali itekeleze mipango mizuri ili kuboresha sekta ya maji kisha atokee mtendaji wa chini kukwamisha juhudi hizo.
“Washukieni wazimawazima, Rais dk.John Magufuli alivyoingia madarakani aliahidi kutekeleza kuboresha sekta hiyo na kuleta maendeleo,na ana fanyakazi nzuri sasa watendaji wa chini wanaosuasua wana maana gani!!tushirikiane kuonyesha jitihada zinazofanywa na serikali”alieleza Ali.
Ali alielezea maji ni haki ya kila mtu, vyanzo vya maji vitunzwe kwa maslahi ya jamii.
Pia kiongozi huyo za mwenge,aliwataka wananchi kushiriki katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na vitongoji.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo akipokea mwenge wa uhuru alisema ,ukiwa mkoani hapo utakimbizwa kwenye wilaya saba ,halmashauri Tisa ambapo miradi 95 itapitiwa yenye thamani ya zaidi ya sh.Bilioni 40.436.6, kati ya miradi hiyo miradi 61 itakaguliwa,17 itawekwa jiwe la msingi,9 itazinduliwa na 8 itafunguliwa.
Akizungumzia sekta ya maji, Ndikilo alibainisha kuwa asilimia 52 ya watu mkoani humo wanapata huduma ya maji safi na salama na wanaopata maji watu 790,000 sawa na asilimia 67 ya wakazi wote milioni 1.2.
Wakati huo huo ,mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga alisema ,mwenge huo utatembelea miradi nane yenye thamani ya bilioni 5.177.
Mwenge wa Uhuru upo mkoani Pwani ukiwa ni mkoa wa 21 tangu ulipozinduliwa mkoani Njombe .