……………………………………………………………………………
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ametaja mambo manne ya kuzingatiwa katika kuhakikisha hali ya upatikanaji maji katika wilaya ya Ikungi inakuwa ya kuimarika ikiwemo kuhakikisha vijiji kumi vinapata chanzo cha maji cha uhakika.
Akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji Mei 7 bungeni ametaja vijiji hivyo kuwa ni Ntuntu,Tharu,Mbogho,Mwau,Mahambe,Choda,Manjaru,Tumaini,Matongo na Unyakhanya.
“Nikupongeze Waziri na timu yako kwa kazi nzuri mnayoifanya katika kuhakikisha wananchi wanapata maji,na Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM katika ukurasa wa saba Ibara 9 D kifungu cha kwanza imeeleza wazi katika miaka mitano kuwa itaongeza nguvu katika upatikanaji wa maji,
“Hivyo katika hili kasi inatakiwa iendelee kuongezeka katika kuwekeza zaidi, najua kazi imefanyika na mimi nina ushahidi katika jimbo langu au Wilaya ya Ikungi tumepata bilioni 3.7 kwa mwaka uliopita,safari hii naona wametubana sana kwa wilaya nzima tumepata Bilioni 1.7 ,maana yake kwa hali ya maji tuliyonayo katika wilaya yetu bado tupo chini sana nina amini kunahitajika juhudi kubwa kuongeza fedha kwa ajili ya kuwekeza zaidi,”alisisitiza.
Amesema kupitia fedha hizo Bilioni 2 waliweza kupata maji katika vijiji vya Kipumbuiko,Kinku na Lighwa.
“Kama wanavyosema tuendelee kula mtori nyama ipo chini basi tuna imani kuwa maji tutapata,”aliongeza.
Jambo la pili ni kuhusu usimamizi wa miradi hiyo ili fedha zilizowekezwa ziweze kuleta tija kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.
“Kwenye miradi hii tunawekeza kwa fedha nyingi lakini tunaenda kuacha kwenye kamati za maji ambazo hazina uwezo kabisa wa kusimamia,lakini pia tumekuwa tuna upungufu mkubwa wa mafundi wanaosimamia miradi hii,pia kumekuwa na urasimu ,unakuta fundi anaagizwa aje asaidie wananchi lakini anaenda pale anaomba hela ya mafuta,”alisema.
Kutokana na hilo ameomba kufanyike marekebisho katika eneo hilo pamoja na kwamba sheria iliyoanzisha kamati za maji ni nzuri kutokana na ushirikishwaji wake lakini inapaswa kuangaliwa upya.
Jambo la tatu Mtaturu ameomba kuanzishwa kwa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Ikungi ili kurahisisha upatikanaji wa fedha katika utekelezaji wa miradi ya maji.
“Katika eneo la Ikungi tulioomba Mamlaka ya maji ya mji wa Ikungi,na ombi hili tulishalitoa miaka miwili iliyopita,tunaamini tukiwa nayo itatusaidia kuwa na uwezo wa upatikanaji wa fedha zingine,tunaomba Waziri ukija hapa tuambie ni lini tutapata mamlaka hiyo ili iongeze kasi ya upatikanaji wa fedha katika kutekeleza miradi na usimamizi wa maji.”alisisitiza.
Mtaturu ametaja jambo la nne kuwa ni kuongeza uwezo wa uchimbaji wa mabwawa ya maji ili kupunguza tatizo la maji katika maeneo yao hasa kwenye eneo la kunywesha mifugo na hata kufua.
“Ikungi tunapata maji asilimia 52 katika majimbo yote mawili ina maana tupo chini ya lengo la ilani,sasa kama hatujafanya juhudi za makusudi hatuwezi kufika ,maeneo hayo watu wanashiriki kunywa maji na mifugo hiyo ni hatari sana, niombe sana juhudi ziongezeke katika eneo hilo ili lengo la kumtua mama ndoo ya maji kichwani lifanikiwe,”alisema.