………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
MBUNGE wa Nanyamba, Abdallah Chikota ameishauri Serikali kuanzisha Mamlaka ya Maji ya Mji wa Nanyamba kutokana na halmashauri hiyo kuwa tayari imeshakuwa na hadhi pia imesajiliwa na sheria ya maji inaruhusu.
Ushauri huo ameutoa leo Mei 7,2021 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Chikota amesema kuwa halmshauri ya mji wa Nanyamba tayari ina hadhi na pia imesajiliwa kama halmashari ya mji na kwa mujibu wa sheria ya maji hivyo wana uwezo wa kuwa na mamlaka yao.
“Naomba Mhe.Waziri hilo jambo ulifanyie kazi tuwe na mamlaka yetu ya mji wa Nanyamba maana tuna kila sababu ya kuwa na mamlaka yetu kutokana na kuwa vigezo vyote, badala ya kuendelea kuhudumia na Mtuwasa,”amesema Mhe.Chikota
Amesema kuwa hali ni tete katika Mkoa wa Mtwara kuhusu suala la maji hata katika kikao kilichopita cha kamati ya ushauri cha mkoa ajenda hiyo iliwekwa maalum.
Hata hivyo amempongeza Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso kwa kukutana na wabunge wa Mtwara na kuwasilikiza na kuanza kulifanyia kazi suala hilo.
Mhe.Chikota ameelezea kuwa walipeleka mambo mawili kwa serikali na kwamba yameshafanyiwa kazi likiwemo la mradi wa maji Makonde ulioondolewa kwenye miji 28 kurejeshwa kwakuwa unahudumia mkoa huo kwa asilimia 40, halmshauri nne ambazo ni Newala Mjini, Newala Vijijini, Tandahimba na Nanyamba.
“Kwahiyo mradi huu ukitekelezwa ipasavyo tutakuwa tumepunguza tatizo la maji katika mkoa wa Mtwara, na nakuomba usikilize ushauri wetu kwamba mradi wa Makonde kupitia chanzo cha mitema kina maji mengi sana utekelezwe,”amesisitiza Mh.Chikota
Aidha ameongeza kuwa kuruhusu matumizi ya maji ya mto Ruvuma kwenda kwenye chanzo cha miembe chini jimboni humo unagusa vijiji 74, na kata 13 za eneo hilo zikiwemo Nanyamba, Mtwara Vijijini na inawezekana ukavutwa na kuingia jimbo la Mtama.
“Mradi huu ukitekelezwa utatatua changamoto nyingi maana mradi wa miembe chini nimesikia hapa kiasi cha sh. bilioni sita kimetengwa hivyo naomba fedha hizo zitolewe kwa wakati”ameongeza