Katibu Mkuu wa TAMUFO,.Stella Joel. |
.
Mlezi wa TAMUFO, Frank Richard |
Na Dotto Mwaibale
UMOJA wa Wanamuziki Tanzania ( TAMUFO) imeliomba Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuhakikisha linashirikisha wadau wa muziki kabla ya kutoa maamuzi ya kuwabana wasanii.
Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa TAMUFO,.Stella Joel jijini Arusha jana baada ya kutokea malalamiko ya wanamuziki kulalamikia kitendo cha Basata kuweka utaratibu wa kuwataka wanamuziki nyimbo zao zikaguliwe baada ya kurekodi kwa sababu za kimaadili.
” Jambo hilo ni kuwaumiza wanamuziki wa Tanzania ambao wanahangaika sana kuwezakumudu gharama za kurekodi kazi zao.” alisema Joel.
Joel alisema wanamuziki wengi hawana kipato cha kutosha na kurudia rudia katika kurekodi kazi zao na bado hawajaweza kufaidika nazo.
Mlezi wa TAMUFO, Frank Richard, ameiomba Serikali kuziwezesha taasisi zenye nia ya kusaidia maendeleo ya sanaa hapa nchini Ikiwemo Basata.
Richard aliomba kuwepo na
utaratibu wa kuandaa semina kwa ajili ya kutoa elimu ya kuwajengea uelewa wasanii juu ya kazi zinazokubalika kimaadili na katika kulinda heshima ya muziki na utamaduni wa Tanzania.
Aidha Richard ameomba Serikali kuhakikisha idadi ya studio zote hapa nchini zinajulikana ili kuweza kutoa elimu kupitia vipeperushi vinavyozungumzia maadali na taratibu zinapaswa kufuatwa kabla ya kutoa wimbo.
Alisema hali hiyo itaepusha hasara zinazosabisha msanii kurudia wimbo pia kuepusha malalamiko hayo yanayojitokeza.
Richard alisema taasisi zinazosimamia kazi za sanaa na wasanii kwa Ujumla ni muhimu ziandae vipindi vya Redio na Tv na mitandao ya Kijamii kwa ajilo ya kutoa elimu kwa wasanii na wamiliki wa studio ili kuwajengea uelewa juu ya jambo hilo.