*********************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti ameipongeza jamii ya wafugaji wa Wilaya ya Simanjiro kuweka kipaumbele kwenye elimu na kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule tofauti na awali walivyokuwa wanapeleka kuchunga mifugo.
Mkirikiti ameyasema hayo wakati akikagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu sita ya vyoo vya shule ya msingi Losokonoi wilayani Simanjiro.
Amesema wanafunzi wa jamii ya wafugaji wa wilaya hiyo hivi sasa wanaona elimu ni kipaumbele japokuwa wengi wao hutembea umbali mrefu kwenda shule na kurudi nyumbani.
Amempongeza mwalimu mkuu wa shule ya msingi Losokonoi Rajab Jabiri kwa ufaulu mzuri wa darasa la saba kwa mwaka jana na akaagiza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Yefred Myenzi na Mwenyekiti wake Baraka Kanunga wamkabidhi zawadi ya mbuzi.
“Juhudi za mwalimu mkuu wa shule ya msingi Losokonoi zinaonekana kwenye ufaulu kwa mwaka jana kwani kati ya wanafunzi 17 waliofanya mtihani wa kuhitimu wanafunzi 14 walifaulu kwenda sekondari hii ni hatua kubwa sana,” amesema Mkirikiti.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Losokonoi Rajabu Jabir amesema shule hiyo ina wanafunzi 308 ikiwa na wavulana 189 na wasichana 119, walimu sita ambao ni wanaume pekee.
Mwalimu Jabir amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2014 ikiwa na vyumba viwili vya madarasa hadi mwaka 2020 kukiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba.
Amesema awali wanafunzi waliweza kupata taaluma yao hadi chini ya vivuli vya miti kwa kukosa vyumba vya kujisomea hivyo mvua, jua na upepo vilikuwa ni adha kwao.
Amesema Juni 26 mwaka 2020 serikali iliwapatia sh86.6 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu sita ya vyoo kupitia mradi wa EP4R.
“Kwa kushirikiana kwa pamoja tulijitahidi kujenga vyumba vinne vya madarasa na ofisi moja ikiwa kila darasa lina madawati 20 na ofisi ikiwa na meza tano na viti 10 na kujenga matundu sita vya vyoo,” amesema mwalimu Jabir.
Amesema wana changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kuwa mbali kiasi cha kilomita 95 hadi 100 na uhaba mkubwa wa maji na zipo jitihada za umaliziaji wa vyumba vitatu vya madarasa ambayo vimefikia hatua ya lenta.
Ameishukuru Serikali akiwemo mkuu wa mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti, Mkuu wa wilaya mhandisi Zephania Chaula, Mkurugenzi mtendaji Yefred Myenzi na timu ya idara ya elimu na ujenzi kwa kuwatembelea na kuwahamasisha.