Mkuu wa Wilaya ya Nyamagna, Dk. Philisi Nyimbi, akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi cha Watu Wenye Ulemavu Mirongo, walimu na wataalamu wa Kata ya Mirongo (hawapo pichani) jana
Mariamu Hamis anayesoma fani ya ushonaji katika Chuo cha Ufundi cha Watu Wenye Ulemavu Mirongo, akipokea mdaftari tisa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana jana.Madaftari hayo yalitolewa na na Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Alhaji Sibtain Meghjee wa tatu kutoka kushoto.
Mwanafunzi Fred Thomas wa fani ya umeme katika Chuo cha Ufundi cha Watu Wenye Walemavu Mirongo, jana akipokea madaftari tisa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamgana, Dk. Philisi Nyimbi,yaliyotolewa na Taasisi ya Desk & Chair Foundation kwa wanafunzi 24 wanaofadhiliwa na taasisi hiyo.
Mama mzazi wa Deogratius Deus, Scolastica Magadula akitoa shukurani kwa uongozi wa Chuo cha Ufundi cha Watu Wenye Ulemavu Mirongo kwa kumtunuku mwanaye cherehani na vifaa vingine vya ushonaji ili aweze kujiajiri.Picha zote na Baltazar Mashaka
…………………………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
TAASISI ya The Desk & Chair Fundation (TD&CF)imetumia sh. milioni 12 kugharamia ada na vifaa vya masomo kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi cha Watu Wenye Ulemavu Mirongo,kulipa deni la Ankara ya umeme na kuchimba kisima cha maji.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo,Alhaji Sibtain Meghjee, alisema jana wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya ushonaji kwa wahitimu wawili kati ya wanne wa fani ya ushonaji hafla ambayo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Dk. Philis Nyimbi.
Alhaji Meghjee alisema wanafanya shughuli za kijamii, wakiwemo watu wenye ulemavu ambapo walipata maombi ya kuwafadhili wanafunzi 24 wa fani mbalimbali na wametumia sh. milioni 12 kuwagharamia ada,vifaa vya masomo,kuchimba kisima cha maji na kulipa deni la sh.350,000 za Ankara ya umeme.
“Tunaipongeza serikali kwa jitihada za kuwapa watu wenye ulemavu elimu na ujuzi kisha wajiajiri baada ya kuhitimu masomo,hapa tumewachimbia kisima cha maji na tunaomba maabara ya maji kupima sampuli ya maji hayo kuona kama yanafaa kwa matumizi ya binadamu au shughuli nyingine,”alisema.
Kwa mujibu wa Alhaji Meghjee wataboresha na kukarabati baadhi ya miundombinu ya chuo hicho yakiwemo mabweni, vyoo na darasa moja ili kukifanya kuwa katika hali na mazingira bora na kuwawezesha watoto wanaotoka mbali kuishi chuoni na watafunga pampu ya umeme au mionzi ya jua ili kusukuma maji kwa ajili ya matumizi ya chuo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Mwanza,Alfred Kapole,alisema mchango wa serikali wa kuendelea kuwathamini watu wenye ulemavu wanauthamini na anafarijika kwa namna taasisi ya The Desk & Chair ilivyowatendea wanafunzi wa chuo cha Ufundi Mirongo.
“Taasisi hii imekuwa karibu na watu wenye ulemavu na hatukutarajia chuo hiki kufunguliwa,leo watoto wanasoma.Mwenyekiti nikupongeze kwa dhati kwa ufadhili huo , ni heshima ya pekee, Mwenyezi Mungu akuzidishie ulipotoa,”alisema.
Kapole alisema watu wenye ulemavu kupata nafasi kwenye chuo hiki ni fursa,kwa sababu ya changamoto ya ukosefu mkubwa wa ajira na kuwataka wasome ili wajiajiri baada ya kuhitimu.
Akizungumza kwenye hafla hiyo,Dk.Nyimbi aliipongeza The Desk & Chair Foundation kwa inavyojitoa na imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya jamii kutokana na misaada inayotoa kwenye sekta ya elimu, afya na maji mkoani Mwanza na maeneo mengine nchini.
“Taasisi hii inaunga mkono juhudi za serikali na tuna kila sababu ya kuthamini mchango mkubwa inaoutoa kwenye jamii ya Watanzania ambao wanaendelea kunufaika na kuwa na tija,”alisema na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya sita inaendelea kuboresha masuala mengi ili kila mmoja anufaike.
Alitoa rai kwa wadau wengine waone nini cha kufanya kwa ajili ya chuo utatuzi wa changamoto za hicho cha Watu wenye Ulemamvu kwani kutoa ni moyo watakaoguswa wamwone Kaimu Mkuu wa Chuo.
Awali Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Watu wenye Ulemavu Mirongo, Harieth Mcharo alisema kukosekana kwa walimu kwa sababu mbalimbali kulisababisha chuo hicho kinachofundisha fani za useremala,ushonaji,uchomeleaji wa vyuma na umeme wa majumbani kufungwa mwaka 2010 kabla ya kufunguliwa ambapo kupitia wadau kimepokea wanafunzi 30.