Kaimu Katibu mtendaji Latra ccc Bw.Leo Ngowi akizungumza na waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya watu wasioona Tanzania Bw.Omary Itambu akizungumza na waandishi wa habari
****************
Baraza la Ushauri la Watumiaji huduma za Usafiri Ardhini (Latra ccc) limewataka watumiaji wa huduma za usafiri kutambua kuwa baraza hilo lipo kwaajili ya kuwakilisha maoni ya watumiaji wa huduma hizo za usafiri ardhini nchini.
Watumiaji wa Usafiri Barabarani wanakutana na changamoto nyingi zikiwemo upandishaji holela wa nauli, kupewa tiketi zisizokuwa na sifa na matatizo kadha wa kadha. Baraza hilo,lipo kwa ajili ya kuwakilisha maoni ya Watumiaji wa huduma, lengo likiwa ni kuhakikisha abiria wote wanaopata huduma bora na salama katika sekta ya Usafiri ardhini Nchini.
Hayo yamesemwa na Leo Ngowi Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri Watumiaji huduma za Usafiri Ardhini akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za baraza hilo zilizopo Kwenye Jengo la NSSF water front ghorofa ya saba jijini Dar es salaam.
Ngowi amesema kuwa kwa kutambua miongoni mwa majukumu ya baraza ikiwa ni kukaa na makundi mbalimbali,kutathimini mwenendo halisi wa utoaji huduma na upokeaji wa huduma hizo ambazo wananchi wanazipata wameamua kukutana na watu wasioona kukaa nao kutafakari kwa pamoja juu ya changamoto wanazokutana nazo katika sekta ya usafiri wa umma kisha kutoa mafunzo maalumu kuhusiana na matumizi ya mfumo wa tiketi mtandao kwa watu wasioona. Amesema, sekta ya Usafiri Nchini ni muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi. Na ili Jamii ya Kitanzania iweze kufikia malengo ya kukua kiuchumi, hatuna budi kuimarisha matumizi ya teknologia katika kukata tiketi kwenye vyombo vyote vya usafiri wa umma Nchini.
Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza la ushauri watumiaji huduma za usafiri Ardhini Leo Ngowi ameongeza kjwa kusema kuwa mafunzo hayo yatafanyika Jijini Dar es salaam Siku ya Ijumaa tarehe 07/05/2021 kuanzia saa tatu kamili asubuhi hadi saa sita mchana katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani Cha Magufuli kilichopo Mbezi luis jijini Dar es salaam ambapo anaamini mafunzo hayo yatasaidia kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo watu wasioona kama vile kubambikiwa nauli za mabasi,usumbufu wanaokutana nao hasa wakienda kukata tiketi inawalazimu kuwa na mtu mwingine anaesindikiza ambapo lazima agharamikiwe nauli ya kwenda na kurudi hivyo kwa kutumia tiketi mtandao inamsaidia mtu asioona kukata tiketi akiwa nyumbani.
Amesema mafunzo hayo kwa Dar es salaam yatatolewa kwa watu wasioona sabini ambapo kundi hilo baada ya kupata mafunzo hayo watakuwa walimu kwa wenzao ambapo yamelenga mambo makubwa manne yakiwemo kufahamu baraza linafanya nini kisheria,kutaka watu wasioona watambue wajibu na haki ya abiria anapokuwa kwenye chombo cha usafiri pamoja na namna ya kutumia tiketi mtandao.
leo Ngowi amesema mafunzo haya ni kwa Tanzania nzima kwa ujumla na kwakuanzia yataanzia Dar es salaam kisha Dodoma na baada ya hapo utaratibu kwa mikoa mingine utaendelea na kuwataka watu wasioona wajiandae na kujitokeza kwa wingi kupata mafunzo hayo.
Kwa upande wake Omary Itambu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Wasioona Tanzania amesisitiza kuwa, ni muhimu jamii yote ikasisitizwa juu ya matumizi ya tiketi mtandao, na kumwomba Mh. Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan kutilia mkazo katika jambo hili, ili kusaidia wananchi wote kupata huduma bila kulanguliwa, na kuwa na uhakika wa taarifa sahihi za abiria kwenye vyombo vya usafiri Nchini.