…………………………………………………………………………..
Mabingwa wa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara timu ya Simba imefanikiwa kuwafuata Watani zao Yanga SC katika hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wageni Kagera Sugara uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Wageni walienda mapumziko wakiwa wanaongoza bao moja lililofungwa na Erick Mwijage dakika ya 45 kwa kichwa baada ya kupokea krosi ya beki Dickson Mhilu.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko wakimtoa Taddeo Lwanga na nafasi yake ikichukuliwa na Bernard Morrison,kuingia kwa mchezaji huyu kulibadilisha mchezo na Simba kuanza kulisakama lango la Kagera Sugar kama nyuki.
Morrison aliwanyanyua mashabiki wa Simba dakika ya 55 akifunga bao safi la kusawazisha na dakika ya 67 Mshambuliaji hatari Meddie Kagere alipigilia msumari wa pili.
Kwa ushindi huo Simba inaungana na vigogo wa Soka nchini Yanga ambao walitinga jana baada ya kuwachapa bao 1-0 Tanzania Prisons Mjini Sumbawanga.