Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara Regina Ndege, akizungumza katika Baraza la Jumuiya ya UWT Wilayani Simanjiro.
******************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MBUNGE wa Viti Maaalum Mkoani Manyara Regina Ndege amewataka wanawake mkoani humo kuhakikisha wanaitumia asilimia nne kati ya 10 ya wanawake kwa wanabuni na kuanzisha miradi itakayostawi na kuleta tija katika kuwaimarisha na hatimaye kuwainua kiuchumi na kujikomboa na umaskini.
Kufuatia hilo Mbunge huyo amewataka wanawake Mkoani humo kuhakikisha wanachangamkia fursa ya kukopa ile asilimia 10 ya wanawake, vijana na walemavu itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuweza kujikwamua kiuchumi, pamoja na kuithamini miradi hiyo kwani ni msaada mkubwa kwao.
Ndege amesema hayo wakati akizungumza kwenye Baraza la Jumuiya ya Wanawake Tanzania ( UWT ) Wilaya ya Simanjiro lililofanyika katika ukumbi wa CCM mbele ya Mwenyekiti wa UWT Wilaya hiyo Agnes Brown Ole Suya na katibu wake Zaria Mwinyi, ambapo alisema hiyo ni fursa inayotakiwa kuchangamkiwa ili wanawake waweze kujiimarisha kiuchumi.
“Lakini hata vikundi vichache vya wanawake vinavyopata hiyo mikopo ya asilimia 10 itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri zetu bado miradi wanayoibua na kuanzisha haistawi kabisa na kuwaletea maendeleo, kwani miradi mingi inakufa, pesa zinapotea, wanawake wanabaki kudaiwa na kubakia kwenye shida moja kwa moja,” amesema mbunge huyo.
Amewataka kubuni kuanzisha miradini vema hata wakawashirikisha wataalam watakaoweza kuwasaidia kubuni miradi itakayoendana na mazingira halisi ya sehemu husika badala tu ya kuamua kuanzisha miradi isiyokua na mwendelezo mzuri na kuwakosesha mapato yao.
” Kubuni na kuanzisha miradi sio tatizo wala sio kazi kubwa, kikubwa ni usimamizi maana miradi mingi inakufa Kwa kukosa usimamizi mzuri, lakini pia kupata eneo zuri la mradi husika utakaoendana na maeneo uliopo, lakini pia huo mradi unatakiwa uthaminiwe yaani iyo kabla ya kuanzisha biashara yoyote ni vema kwanza ukatafakari namna mradi huo itakavyosimamiwa ili kuweza kuleta tija katika mapato yatakayopatikana,” ameongeza Mbunge Ndege.
Mbali ya hayo Mbunge Ndege alisema bado hali ya wanawake kiuchumi wako chini sana, hivyo wanahitaji kusaidiwa na namna pekee ya kusaidiwa ni kupewa nguvu katika kuibua miradi itakayowainua kiuchumi ili maisha yao yaweze kubadilika.
“Hali zetu bado ziko chini mno, yaani ninyi mlikotoka kule akina mama wanaowazunguka bado wako nyuma sana, wanahitaji kusaidiwa, na namna ya kuwasaidiwa ni katika kupitia vikundi ambavyo vinawezeshwa, kuwe na vikundi vya akina mama ambavyo viwezeshwe vipewe nguvu lakini visaidiwe kuibuliwa miradi ambayo itawainua kiuchumi,” alisema Ndege.
Alisema kati ya asilimia 10 ya mkopo unaotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ni asilimia nne tu ndio inayokwenda kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana, huku asilimia mbili ikienda kwa walemavu, hivyo asilimia nne zikigawiwa kwa wanawake hazitatosha kwani ndiyo kundi kubwa na familia nyingi zinatunzwa na akina mama, hivyo inahitajika asilimia hiyo iongezwe ili kuleta tija.
Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania ( UWT ) Wilaya ya Simanjiro Agness Brown Ole Suya aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuhakikisha wanatoa ushirikiano mkubwa kwa mbunge huyo ili aweze kitimiza yale yote aliyoyaahidi wakati wa uchaguzi uliofanyika Julai 23, 2020 juu yao.
Hata hivyo aliongeza kuwa kiongozi yeyote anapopata ushirikiano wa dhati kwa waliompa dhamana, inampa urahisi katika kuwatumikia vema lakini pia kuongeza ufanisi katika kutimiza yale aliyoyakusudia, hivyo ni vema wakatoa ushirikiano mkubwa kwa viongozi hao.