Na Dixon
Busagaga,Arusha
KITUO cha Uwekezaji
nchini (TIC) kimeeleza kuridhishwa na uwekezaji uliofanywa na kampuni ya Grumet
Reserve (T) Ltd ya jijini Arusha ,uwekezaji ambao unatajwa kuwa zaidi ya Bilioni
624 huku ikiwa miongoni mwa mwekezaji mahiri nchini .
Mbali na uwekezaji
uliofanywa na kampuni ya Grumet Reserve Ltd kupitia Hoteli za kitalii zilizopo
katika Hifadhi za taifa kwa ajili ya kuhudumia wageni mashuhuri na wenye hadhi duniani,kampuni hiyo pia imeendelea
kukua na sasa imeanzisha huduma za usafiri wa anga kupitia Grumet Air.
Maafisa kutoka kituo
cha uwekezaji (TIC ) makao makuu wametembelea ofisi za kampuni ya Grumet Reserve
(T) Ltd na kufanya mazungumzo na Meneja uendeshaji wa kampuni hiyo Mark Rashid ikiwa ni sehemu kazi ya kituo hicho kuhamasisha na kusaidia
wawekezaji wa kigeni na watanzania waweze kutumia fursa zilizopo nchini.
Akizungumzia ziara
hiyo Afisa Mhamasishaji Mwandamizi wa kituo cha uwekezaji (TIC) ,Innocent Kahwa
amesema katika kitimiza majukumu ya kituo cha uwekezeji wameanza kutembelea
miradi ambayo inajulikana kama miradi mahiri ambayo imekuwa ikisajiliwa na
kituo hicho.
“Huu mradi unajulikana
kama Grumet Reserves Ldt, ni mradi ambao unaendesha lodge ya kitalii uwekezaji
wake ukiuweka kwenye fedha za kitanzania thamani yake ni sawa na Billion
624,kwa hiyo kuanzia 2005 mpaka sasa hivi tunaweza kuona ni kiasi gani ambacho
kimeweza kuwekezwa na mwekezaji mmoja mahiri ambaye amewekeza hapa nchini.” Alisema
Kahwa
“Huyu mwekezaji ni mahiri na anahudumia wateja watalii wakubwa wenye hadhi duniani, unajua katika sekta ya utalii watalii wamegawanyika wapo wa kiwango cha kawaida, watalii wa kiwango cha kati na watalii wenye kiwango cha juu, kwa hiyo huyu mwekezaji wetu anahudumia watalii wa kiwango cha juu duniani sio kiwango cha juu kwa Tanzania “No” Ni kiwango cha juu duniani” aliongeza Kahwa.
Kahwa alisema kutokana
na kutambua ubora wa huduma ambazo zimekuwa zikitolewa na hoteli zilizopo chini
ya Grumet Reserve Ltd,kampuni hiyo imekuwa ikipokea tuzo mbalimbali duniani ambazo
kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiitangaza Tanzania .
“Kwa mfano mwaka 2011, mwaka 2012, mwaka 2015 na mwaka 2016 iliweza kutambulika kama Hoteli namba moja duniani, na vilevile mwaka 2016 na mwaka huu imeweza kujulikana kuwa ni lodge ya safari namba moja bora kwa Africa.”alisema Kahwa.
“Kwa hiyo hii hoteli ni mradi ambao unaotambulika kwa duniani. Yaweza ikawa hapa Tanzania mradi huu watu hawaujui lakini duniani huu umetupa sifa kama nchi.” Aliongeza Kahwa .
Alisema mradi huo umeweza kutoa ajira ya watu 800 ambao wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali katika kampuni hiyo huku ukilipa kodi na tozo mbalimbali za serikali ambapo tangu kuanza kwake wameweza kulipa kodi Dola Mil 34.1.
Kahwa
alisema wakati kampuni hiyo inaanza ilianza na vitanda 12 katika hoteli yake ambapo kwa sasa
vimefikia vitanda 124 na kwamba imekuwa ikijihusisha na uhifadhi ambapo tayari
wameingiza wanyama 32 aina Faru weusi
ambao ni kivutio kikubwa kwa watalii .
“Tunazidi
kuhimiza na kushawishi wawekezaji wa aina hii waweze kuwa wengi zaidi kwa sababu
wanaongeza pato la kigeni kwa nchi ,wanaongeza mapato,wanatoa ajira na
kuitangaza nchi yetu duniani”.alisema Kahwa.
Ziara ya
maofisa kutoka kituo cha uwekezaji (TIC) makao makuu imehusisha pia Mwanasheria
mwanadamizi wa kituo cha uwekezaji (TIC) Alex Mnyani na Afisa uhamasishaji
uwekezaji ,Linda Loom wote kutoka makao makuu ya TIC .
Mradi wa kampuni ya
Grumet Reserve (T) Ltd ulisajiliwa kituo cha uwekezaji (TIC) mwaka 2005,wakati huo ukiwa na thamani ya
Dola Milioni 18 na sasa umefikia thamani ya Dola za kimarekani Mil 343 baada ya
kufanya vizuri.
Mwisho .