TAMKO UCHAMBUZI WA HOTUBA YA MHE. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA BUNGENI KWA MTIZAMO WA KIJINSIA 24 APRILI 2021
Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uongozi na Uchaguzi, kwa kushirikiana na wadau wengine wanaoshughulika na masuala ya usawa wa jinsia na haki za wanawake, tunayo furaha kubwa kuendelea kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameandika Historia katika nchi yetu na ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke Tanzania.
Halikadhalika, tunampongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujasiri wake wa kupokea Serikali na kuongoza taifa katika kipindi kigumu cha majonzi baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amin.
Sisi, Wanamtandao tunaoshugulika kutetea na kukuza uongozi uliojengeka katika misingi ya haki na usawa wa jinsia, tumemfuatilia kwa karibu Mheshimiwa Rais akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu aapishwe tarehe 19 Machi 2021 na kutoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hotuba hii imeonesha vipaumbele ambavyo vimegusa maeneo mbalimbali ya maendeleo katika nchi yetu, yakiwemo yale ya kuneemesha maisha, haki, na usawa katika makundi mbalimbali ya kijamii.
Kipekee tumefurahishwa na Mheshimiwa Rais Samia kwa kuonesha bayana tunu za kuongoza taifa ambazo zimejumuisha masuala ya haki, demokrasia, na usawa.
Ni matumaini yetu kuwa tunu hizi muhimu zikidumishwa, kulindwa na kutetewa, zitatoa mwanga mkubwa katika kuongoza utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya sita, ambavyo vimejumuisha kukuza uchumi na kupambana na umasikini nchini, kupambana na rushwa na ubaridhifu wa mali ya umma, ulipaji wa kodi usio na bughudha, kukuza na kuongeza tija katika sekta ya kilimo na mifugo, kukuza ajira na mapato kwa kukuza na kulinda sekta ya Madini, utalii, viwanda na kwingineko, kuendeleza na kukuza miundo mbinu mbalimbali, kuboresha na kuleta mapinduzi zaidi ya teknolojia, TEHAMA na mawasiliano, kuongezea uwekezaji katika sekta za nishati, elimu, afya (na haswa afya ya uzazi), kukuza na kudumisha misingi ya demokrasia, amani na uhuru, na zaidi kuhakikisha misingi ya haki na sheria zinatumika kulinda wananchi.
Tunapenda kusisitiza kuwa, katika uchambuzi wetu kuhusu Hotuba hii ya kwanza ya Mhe. Rais Samia, unaonesha kuwa maeneo yote yaliyopewa kipaumbele katika Serikali yake, yanatoa fursa kubwa ya kukuza maendeleo yatakayowafikia na kuwanufaisha wanawake, wasichana na makundi mengi mengi ya wanyonge nchini, kama utekelezaji wa vipaumbele hivi utajengeka na kutekelezeka katika misingi ya haki na usawa, ukiwemo usawa wa jinsia.
Kwa kutumia mifano michache tu hapo chini, tunaonesha jinsi maeneo yaliyobainishwa na Mheshimiwa Rais yanavyotoa fursa za kukuza misingi na matokeo ya maendeleo yatakayopelekea kukua kwa misingi inayojumuisha usawa wa jinsia, na kwa uhakika Mhe. Samia Suluhu Hassan anastahili pongezi kwa hayo:
i) Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa ahadi ya kulinda misingi ya demokrasia na uhuru wa watu pamoja na wanasiasa na vyombo vya habari.
Katika utekelezaji wa hili, tunaona fursa kubwa ya kujenga misingi na mikakati ambayo haitaacha nyuma ushiriki na sauti za wanawake kama wanajamii wa Taifa hili.
Hivyo, tunamuomba Mheshimiwa Rais kwamba katika kukutana na vyama vya siasa, kuwe na msisitizo wa kuhakikisha mkakati wa usawa wa jinsia na demokrasia ndani ya vyama inatekelezwa kama ajenda yao kimkakati.
ii) Kipaumbele cha kuboresha Sekta ya madini, utalii na nyinginezo ni cha kupongezwa sana. Kwa bahati mbaya, kwa muda mrefu sekta hizi zimekuwa zikitoa kipaumbele na kuwanufaisha zaidi wanaume kuliko wanawake. Ni matumaini yetu kuwa utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamuya Sita, utatilia mkazo kuhakikisha kuwa wanawake wananufaika na fursa zitokanazo na sekta hizo.
iii) Juhudi za kuboresha kilimo ili kufungamanisha maendeleo ya kilimo na viwanda kwa lengo la kuwezesha mazao ya kilimo yatumike kama malighafi za viwanda. Jambo hili litasaidia wakulima, wakiwemo wakulima wanawake vijijini kuweza kuuza mazao yao viwandani na kununua bidhaa za viwandani.
iv) Kutoa kipaumbele katika uwekezaji, na umiliki wa ardhi ni suala nyeti na tete ambalo linahitaji umakini mkubwa. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuainisha kipaumbele hiki na kuahidi kuwa ushiriki wa wanawake katika suala hili ni wa muhimu sana kwani ardhi imekuwa msingi mkuu wa ushiriki wa wanawake katika maendeleo. Tunatarajia kwamba wanawake ambao wamekuwa wakilisha taifa hili kwa muda mrefu watapewa kipaumbele katika fursa zitokanazo na kilimo cha biashara tofauti na walivyokuwa wakiachwa nyuma kwa muda mrefu.
v) Kuongeza usawa wa kijinsia kwa kuongeza wanawake wengi zaidi katika nafasi za uongozi kwa kuzingatia vigezo na sifa stahiki. Juhudi hizi zitapunguza pengo la usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi na kuongeza tija katika kuingiza masuala ya kijinsia katika sera, bajeti, mipango na michakato yote ya maendeleo. Hii itasaidia katika kuongeza kasi ya maendeleo jumuishi na endelevu nchini.
vi) Kuongeza juhudi katika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto. Pia, kuimarisha huduma za afya kwa kujenga miundo mbinu, kuongeza watumishi, vifaa-tiba, dawa na vitendanishi, pamoja na kuboresha Bima ya afya kwa wazee na kwa wote. Juhudi hizi zitawasaidia wanawake kwani ndio wanaobeba mzigo mzito katika masuala ya afya katika familia na jamii kwa ujumla.
vii) Kuongeza uwajibikaji wa watendaji katika miradi ya maji, kuhakikisha upatikanaji wa maji sehemu zisizo na maji kwa kupitia mabwawa ya kuvuna maji ya mvua na kuimarisha kamati za maji za mitaa na vijiji ili ziweze kutimiza majukumu yao kwa ufanisi. Juhudi hizi zitawapunguzia wanawake mzigo wa kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kutumia muda huo kwenye shughuli za uzalishaji.
viii) Kuboresha mfumo wa elimu nchini kwa kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Ufundi ya mwaka 2014 na mitaaala ya elimu ili iendane na muktadha wa sasa.
Tunatarajia mapitio haya yatakuwa jumuishi na yatatoa kipaumbele kwa watoto wa kike na wenye ulemavu ili waweze kunufaika na haki yao ya msingi ya kupata elimu bora.
Sisi wanamtandao tunaahidi kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Awamu ya Sita kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa ushirikiano kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Awamu ya Sita katika kufuatilia na kutoa ushauri juu ya utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa katika hotuba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Imetolewa na:
Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uongozi, na Uchaguzi.