Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Morogoro Mhandisi Nkolante Ntije (wa kwanza kulia), alipokuwa akikagua Daraja la Mto Ruvu eneo la Kibungu Chini katika barabara ya Bigwa hadi Kisaki (km. 133.6).
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Morogoro Mhandisi Nnkolante Ntije (watatu kutoka kushoto), wakati akikagua barabara ya Bigwa hadi Kisaki, Sehemu ya Bigwa Kiswira/Msalabani Kilometa 50, inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (kulia), pamoja na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Morogoro Mhandisi Nnkolante Ntije (kushoto), wakiangalia hali ya Daraja la Mto Ruvu (halipo pichani), katika barabara ya Bigwa hadi Kiswira Kilometa 50 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami
Muonekano wa Daraja la Mto Ruvu, eneo la Kibungo Chini katika barabara ya Bigwa hadi Kiswira Kilometa 50 ambalo litaondolewa na kujengwa daraja jipya litakalo kuwa na uwezo wa kupitisha magari pande zote mbili kwa wakati mmoja.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya akipokea zawadi ya matunda aina ya mashelisheli kutoka kwa mkazi wa kijiji cha Matombo eneo la Msalabani mkoa wa Morogoro, mara baada ya kumaliza kukagua barabara ya Bigwa hadi Kiswira Kilometa 50 itakayojengwa kwa kiwango cha lami.
************************
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, ametembelea na kukagua barabara ya Bigwa hadi Kisaki iliyoko mkoani Morogoro yenye urefu wa kilometa 133.28, ambayo tayari ilishafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, tangu mwaka 2017 na Kampuni ya Mshauri M/s Unitec Civil Consultant ya Tanzania kwa ushirikiano na Kampuni ya Multi Tech (PTY) Ltd ya nchini Borswana.
Akiongea na waandishi wa habari katika daraja la mto Ruvu, eneo la Kibungo Chini, kwenye barabara hiyo ya Bigwa hadi Kisaki, Naibu Waziri Kasekenya alisema kuwa amefika katika barabara hiyo kufuatia ahadi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ya kuijenga barabara hiyo kilometa 40 kwa kiwango cha lami.
Itakumbukwa kuwa Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamisi Taletale alimuomba Hayati Dkt. Magufuli alipokuwa akifungua soko la Kingalu mwezi Februari mwaka huu, kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami kutokana na umuhimu wake katika usafirishaji wa mazao ya chakula, matunda na mbogamboga unaofanywa na wakulima wa maeneo ya Mvuha, Matombo na maeneo jirani, lakini pia ni barabara pekee inayoiunganisha mkoa wa Morogoro na Stesheni ya Tazara ya Kisaki”. Amesema Mhandisi Kasekenya
Ameongeza kuwa, ahadi za Hayati Dr. Magufuli zinaendelea kutekelezwa chini ya uongozi mahiri wa Raisi wa awamu ya sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kama ambavyo amekuwa akijipambanua kupitia salamu yake na kauli mbiu yake isemayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi iendelee na kwamba ni kweli kazi zinaendelea kutekelezwa, hazitasimama.
Nae Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Morogoro Mhandisi Nkolante Ntije, amewaambia waandishi wa habari kuwa, ofisi yake iko tayari kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ya Bigwa hadi Kisaki sehemu ya Bigwa hadi Kiswira Kilometa 50 badala ya Kilometa 40 za awali kufuatia maombi ya Serekali ya mkoa wa Morogoro.
Niwatoe hofu wananchi wa maeneo yaliyopitiwa na mradi huu kwakua mradi hautachukua muda mrefu hivyo basi wajiandae na wasiwe na wasiwasi kwasababu sheria, kanuni na taratibu za fidia zitafuatwa kwa maeneo ambayo yatatwaliwa kutokana na kuwa nje ya hifadhi ya barabara. Amesisitiza Mhandisi Ntije
Naibu Waziri Kasekenya yuko Mkoani Morogoro kwa zira ya kikazi ya siku mbili, ili kukagua miundombinu ya barabara iliyoharibika kutokana na mafuriko yatokanayo na mvua zinazoendelea mkoani humo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi