*******************************
Dar es Salaam, 21 Aprili 2021:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa kuhusu kimbunga Jobo kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.
Kumejitokeza mgandamizo mdogo wa hewa ambao umefikia kiwango cha kimbunga hafifu kwa jina Jobo. Kimbunga hicho kipo kaskazini mwa Kisiwa cha Madagascar katika Bahari ya Hindi umbali wa Kilometa 930 na kilometa 1030 kutoka pwani ya Lindi na Mtwara. Aidha, uwepo wa kimbunga hicho unatarajiwa kusababisha ongezeko la upepo na mawimbi katika bahari ya Hindi hususan katika Pwani ya mwambao wa mikoa ya Mtwara na Lindi.
Mamlaka inaendelea kufuatiliia mwenendo na mwelekeo wa kimbunga Jobo kwa kuzingatia mifumo mingine ya hali ya hewa iliyo jirani zaidi na kimbunga hicho ambayo inaweza kubadili nguvu na mwelekeo wa kimbunga Jobo katika wakati ujao.
Wananchi waendelee kuzingatia tahadhari ya upepo na mawimbi iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania katika maeneo husika. Mamlaka ya Hali ya Hewa itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.