****************************
Na Mwandishi wetu, Babati
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara kwa kipindi cha miezi mitatu ya Januari hadi Machi mwaka huu imefuatilia miradi 19 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.87 iliyopo Mkoani humo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo Mjini Babati wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa kipindi cha miezi mitatu ya ufanyaji kazi wa Taasisi hiyo.
Makungu amesema wamefuatilia miradi hiyo ili kuhakikisha wanadhibiti ubora wa thamani ya fedha ukilinganisha na utekelezaji wa miradi yenyewe.
Ametaja miradi hiyo ni ujenzi wa madarasa mawili na matundu saba ya vyoo vya shule ya msingi Hangoni wenye thamani ya shilingi milioni 47.7 na ujenzi wa bweni la shule ya sekondari Babati wa thamani ya shilingi milioni 80.
Amesema miradi mingine ni ujenzi wa madarasa mawili na vyoo matundu saba ya shule ya msingi Sinai wa shilingi milioni 47.7 na mradi wa maji Tsamas wa thamani ya shilingi 549,433,700.00.
“Miingine ni mradi ni wa Maji Gidas wa thamani ya shilingi milioni 354,7 na ujenzi wa madarasa matatu na matundu sita ya vyoo vya shule ya msingi Darajani wa thamani ya shilingi milioni 60. ” amesema Makungu.
Amesema miradi mingine ni maji vijiji vya Mawemairo, Shaurimoyo na Giring’war wa thamani ya shilingi milioni 203.2 na ujenzi wa madarasa matatu ya shule ya msingi Dosidosi wa shilingi milioni 66.6.
Ametaja miradi mingine ni ujenzi wa shule ya msingi Lalaji wa shilingi milioni 700 na ujenzi wa choo cha wanafunzi wa na vyumba vinne vya madarasa ya shule ya msingi Kaloleni wa thamani ya shilingi milioni 47.700.
“Miradi mingine ni ujenzi wa miundombinu ya shule ya msingi Mulbadaw wa thamani ya shilingi milioni 236.5 na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za mfuko wa kaya masikini TASAF katika halmashauri za wilaya ya Babati, Kiteto, Mbulu, Hanang’ na Simanjiro,” amesema.
Amesema katika uelimishaji wa umma wamefanikiwa kuendesha semina 10 kwa makundi tofauti ya jamii katika kupambana na rushwa.
Amesema mikutano tisa ilifanyika ikiwa na madhumuni ya kuelekeza athari za rushwa na namna ya kupambana nayo kupitia utaratibu wa TAKUKURU inayotembea kwa kuwafuata wananchi katika vijiji ambavyo vipo tayari na wakiwajulisha wanawapa upendeleo.
“Jumla ya klabu 62 za wapinga rushwa katika shule za sekondari zilitembelewa kwa lengo la kuziimarisha na kupatiwa mafunzo,” amesema Makungu.