Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Ally Kidunda akiwa ofisini kwake.
*********************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Ally Kidunda amewataka wagombea wa CCM wa nafasi ya wajumbe wa Halmashauri Wilaya, Mkoa na Katibu Mwenezi wa CCM wa wilaya wasichafuane ila waombe kura kistaarabu.
Kidunda ameyesema hayo wakati akielezea maandalizi ya kufanyika kwa kikao cha halmashauri kuu ya CCM ya wilaya hiyo kitakachofanya uchaguzi wa kujaza nafasi tatu.
Amewataka wagombea wa nafasi ya Katibu mwenezi, wajumbe wa halmashauri kuu ya mkoa na wilaya kufanya kampeni bila kuchafuana kama desturi ya chama hicho.
Amesema anatoa angalizo kwa wagombea wote kuwa wastaarabu na kutosemana vibaya na kuchafua majina ya wagombea wengine kwani siyo vizuri.
“Ombi langu kwa wagombea wote kama kilivyo chama chetu tunatarajia ushirikiano kwenu na hivyo msisemane vibaya na msichafuane, fanyeni kampeni ya kistaarabu,” amesema Kidunda.
Amesema kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Simanjiro kitafanya uchaguzi wa nafasi tatu zilizowazi za Katibu mwenezi wa CCM, mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM mkoa na mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya.
“Tunatarajia uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Aprili 25 makao makuu ya wilaya mji mdogo wa Orkesumet na ukumbi utakaofanyika uchaguzi huo tutawatangazia,” amesema Kidunda.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika ili kuziba nafasi zilizo wazi baada ya kutokea vifo na wengine kupata nafasi za uongozi baada ya kuchaguliwa kushika nafasi nyingine.