Meneja Ushirikishwaji wa ECLA Africa Consult, Lauden Cheyo na Mkufunzi mkuu wa mafunzo ya kuandaa taarifa za fedha kwa mfumo wa IPSAS akimkabidhi cheti Beatrice Haule wakati wa kumaliza mafunzo hayo.
Meneja Ushirikishwaji wa ECLA Africa Consult, Lauden Cheyo na Mkufunzi mkuu wa mafunzo ya kuandaa taarifa za fedha kwa mfumo wa IPSAS akimkabidhi cheti Bariki Malugu wakati wa kumaliza mafunzo hayo.
***********************************
Na Mwandishi Wetu.
TAASISI ya ECLA Africa Consult yenye makao makuu yake Jijini Dar es Salaam, inayojihusisha na masuala ya ukaguzi, ushauri wa kifedha na kodi imewatunuku vyeti wahitimu zaidi ya 17 waliokuwa wakijifunza kwa vitendo mbinu ya kuandaa taarifa za fedha kwa kutumia mfumo mpya wa IPSAS (International Public Sector Accounting standards).
Mafunzo hayo kwa wahasibu na wakaguzi kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s),Taasisi za Kidini na Mashirika ya Serikali yamefanyika kufuatia maamuzi ya Bodi ya wahasibu na wakaguzi, ya 22 June 2020 ya kubadili mfumo wa kuandaa taarifa za kifedha kutoka IFRS (International Financial Reporting Standards) kwenda IPSAS.
wakizungumza kando ya mafunzo hayo baadhi ya waliotunukiwa vyeti waliipongeza ECLA Africa Consult huku pia wakiomba kuendelea kutoa mafunzo zaidi siku za usoni.
Silas Nyanda ambaye ni Muhasibu kutoka katika shirika la Kimataifa lenye makao yake Dodoma la Action Against Hunger, amepata kitu kwenye mafunzo hayo ambapo anaamini yataenda kusaidia taasisi yake.
“Elimu haina mwisho. mara nyingi elimu kwa vitendo inaongeza ubora na thamani zaidi hivyo niwashahuri wahasibu wenzangu wengine ambao hawajapata mafunzo haya wajitokeze kwa wingi wataongeza kitu kwenye ofisi zao”. Alisema Nyanda.
Kwa upande wake Georgia Kabantega ambaye ambaye ni mdhibiti wa mahesabu kutoka taasisi binafsi ya DRC (Denish refugees), alieleza kuwa mafunzo hayo kwake yatamsaidia kufanikisha shughuli zake za kihasibu hivyo ametoa wito kwa wahasibu wengine kujitokeza kwa wingi kupata mafunzo hayo.
Nae Meneja Ushirikishwaji wa ECLA Africa Consult, Lauden Cheyo ambaye pia alikuwa mkufunzi mkuu wa mafunzo hayo alisema washiriki wote walioshiriki wameweza kufanya kwa vitendo kupitia mfumo huo mpya wa IPSAS.
“Washiriki wamenufaika sana kwani wameweza kutumia kompyuta zao na kuandaa taarifa za fedha kwa kutumia excel spreadsheet kufuatana na mfumo wa IPSAS.” Alisema Lauden Cheyo.
Aidha, Cheyo alisema kuwa, kwa kuona uhitaji na maombi ya watu wengi, wameandaa mafunzo kama hayo mengine yatakayofanyika 31Mei hadi 4 Juni, mwaka huu.
Kampuni ya ECLA Africa Consult inaamini mafunzo hayo yataenda kuwa chachu kwa wahitimu hao kwa kuwawezesha kuandaa taarifa za fedha zinazokidhi viwango vya mfumo wa mpya wa IPSAS.