************************************
Aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, leo amekabidhi kijiti hicho kwa Ndugu Grayson Msigwa aliyeteuliwa hivi karibuni na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan huku akikumbukia jinsi kazi hiyo ilivyomfanya asilale.
Dkt. Abbasi ambaye amepandishwa cheo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo, pamoja na kazi nyingine, ataendelea kuisimamia na kuisaidia ofisi hiyo ya Msemaji Mkuu, ameeleza waandishi wa habari mjini Dodoma leo wakati wa makabidhiano kuwa kazi hiyo ilimchukua muda mwingi katika saa 24 za siku hivyo ni kazi adhimu na muhimu kwa Taifa.
“Leo Ndugu Msigwa nakukabidhi majukumu haya sisemi ulikotoka ulikuwa unalala, hapana. Ila kazi hii ya Usemaji haulali katika saa 24 na hata ukilala inabidi ulale kimkakati,” alisisitiza Dkt Abbasi ambaye amekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali kwa miaka minne na miezi nane.
Dkt. Abbasi alimpongeza Bw. Msigwa kwa uteuzi huo na kueleza kuwa anaamini atafanikiwa kuendeleza pale yeye alipoishia.
“Nakupongeza Ndugu Msigwa kwa uteuzi huu kutoka kwa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Msemaji Mkuu wetu, tunashukuru sana katika sekta yetu ya habari tumempata kiongozi mwenye taaluma ya habari kwani umekuwa mwandishi wa habari miaka ya nyuma hivyo si mgeni katika eneo hili.”
Aidha, Dkt. Abbasi amemshukuru Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwamini na kumteua mwaka 2016 na amemshukuru pia Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini aendelee kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika uteuzi uliofanyika Aprili 4 mwaka huu.
Kwa upande wake, Bw. Msigwa naye alimshukuru Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua yeye kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu kwa miaka mitano 5 na zaidi na sasa anamshukuru Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kwenye nafasi mpya kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali.
“Nitaweka mikakati jinsi ya kufanya kazi kwa kushirikiana na watendaji pamoja nanyi wadau wa habari. Nampongeza Dkt. Abbasi kwa kazi kubwa aliyoifanya na leo anakuwa bosi wangu ni jambo la kumpongeza sana na najua ninyi wanahabari huwa hampigi makofi lakini kwa hili hebu tumpigie makofi kidogo,” alisema Msigwa.