Mkuu wa shule ya sekondari Mwandet mwalimu John Massawe
akisoma taarifa ya shule hiyo katika mahafali ya nne ya kidato cha sita
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wakiwa katika sherehe ya mahafali yao
………………………………………………………………………………
NA NAMNYA KIVUYO, ARUSHA.
Shule ya sekondari Mwandet iliyodumu kwa miaka mitatu katika nafasi shule kumi bora kitaifa kwa matokeo ya kidato cha sita inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa nyumba za walimu pamoja na maji jambo linalofanya shule hiyo kushindwa kufikia malengo waliyokusudia.
Akisoma risala ya shule katika majafali ya nne ya kidato cha sita mkuu wa shule hiyo mwalimu John Massawe ina malengo ya kuongeza ufaulu na kuwa ya kwanza kitaifa kila mwaka kwa kidato cha sita na kidato cha nne lakini changamoto hizo zimekuwa chanzo cha kupunguza kasi waliyonayo.
Mwalimu Massawe alisema kuwa kwa upande wa nyumba za walimu wana nyumba kwaajili ya walimu 9 pekee huku walimu wakiwa 43 hali inayosababisha walimu walio wengi kukosa kukosa mahali pa kuishi huku maeneo ya karibu na shule kutokuwepo kwa nyumba za kupanga.
“Katika mazingira haya hakuna nyumba za kupanga hivyo walimu wengi wanalazimika kuishi Ngaramtoni na maeneo mengine ya jiji la Arusha na hali huwa tete zaidi kipindi cha mvua ambapo korongo hujaa maji na walimu kukwama kuvuka,” Alisema Mwalimu Massawe.
Kwa upande wa uhaba wa maji alisema kuwa maji wanayoyapata ni kidogo na wakati mwingine hayapatikani kabisa hali inayoilazimu shule kuagiza maji kutoka mjini kwa gharama kubwa na kutukana na matumizi ya shule maji hayo hutumika kwa siku moja tu.
“Tunaagiza maji boza moja kwa shilingi laki mbili na inapelekea kuzidi kwa gharama za uendeshaji wa shule na wakati mwingine wanafunzi wanatoka nje ya shule kwenda kutafuta maji kwaajili ya matumizi yao,”Alisema .
Aidha risala ya wanafunzi wa kidato cha sita ilianisha changamoto ya maji ambapo walisema kuwa changamoto ya maji inawafanya wanafunzi kwenda kutafuta maji nje ya shule na kutumia muda wao wa kujisomea kutafuta maji hali inayoadhiri taaluma yao.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Ilboru Mwl Denis Otieno akimwakilisha mkurugenzi wa halmashauri hiyo alisema kuwa serikali inaendelea kutatua changamoto zilizopo katika shule hiyo kadri fedha zinavyopatikana ambapo baada ya kuwajenge bweni la kisasa, madarasa manne na ofisi yake na choo cha matundu 10 kwaajili ya kidato cha tano na sita, kumalizia bwalo, kujenga maktaba mpya na na kutoa fedha kwaajili ya choo cha wafanyakazi kinachofuata ni nyumba za walimu.
Mwalimu Otieno alisema kuwa kwa upande wa maji wanamradi wa maji unaoendelea katika kijiji cha Losikito kilichopo ndani ya kata hiyo ambao baada ya kukamilika tawi moja litaekekezwa katika shule hiyo.
Nao baadhi ya wazazi waliohudhuria katika mahafali hayo wakiongea na mwandishi wa habari Rehema Obedi na Onesta Alfayo walisema kuwa ni vema wadau mbalimbali wa elimu wakaisaidia shule hiyo kwa kuchangia kujenga nyumba mbalimbali pamoja na kuwaweka Gata za kukinga maji ya mvua kwenye majengo yote ya shule hiyo kuliko kuisubiri serikali peke yake kwani inakazi kubwa ya kutatua changamoto katika maeneo mengi.
“Tukihisubiri serikali peke yake, tunajua itafanya lakini sio kwa haraka kutokana na majukumu makubwa iliyonayo lakini wananchi wenye kupenda maendeleo ya elimu wakiamua wanaweza kuondoa changamoto hizi ndani ya muda mfupi kwahiyo sisi tuwaombe wote watakaoguswa wasaidie malengo ya shule hii na ndoto za wanafunzi hawa ziweze kutimia na hasa wanafunzi wa kidato cha sita ambao ni wasichana tuu.
Hata hivyo shule hiyo ilianzishwa mwaka 2004 ikiwa na wanafunzi 28 na ikiwa na mazingira magumu ya madarasa mawili na nyumba moja ya walimu ambayo ilikuwa haijakamilika ambapo kwa sasa shule ina wanafunzo 1316 wavulana wakiwa 491 na wasichana 825 na pia shule hiyo imefanikiwa kuanzisha elimu ya sekondari ya juu 2016 na wana tahasusi mbili ambazo ni HKL na HGK.
Kuhusiana na maendeleo ya shule kwa elimu ya sekondari ya chini (O’Level) mwaka 2018 walikuwa na daraja la kwanza 7, daraja la pili 17, la tatu 58 la nne 131 na sifuri 35 ambapo kwa mwaka 2019 daraja la kwanza ni 2, la pili 41, la tatu 65 la 175 na sifuri 36 na mwaka 2020 daraja la kwanza ni 16, la pili 61, la tatu 53, la nne 148 na sifuri 12 na kwa mwaka 2021 wana lengo la kuondoka daraja sifuri.
Taaluma upande wa elimu ya sekondari ya juu ( A’ Level) kwa mwaka 2018 kulikuwa na daraja la kwanza 26 na daraja la pili 3 hali iliyoifanya shule hiyo kuwa kuwa ya kwanza kimkoa na ya pili kitaifa kwa shule zenye watahiniwa chini ya 30.
Mwaka 2019 daraja la kwanza zilikuwa 70, la pili 6 na kuifanya shule kuwa ya pili kimkoa na ya nne kitaifa huku mwaka 2020 ikiwa na daraja la kwanza 37 na la pili 6 na kuifanya shule kuwa ya tatu kimkoa na ya tisa kitaifa ambapo wanalengo la kuendelea kubaki katika nafasi ya shule bora kitaifa.