TIMU ya Polisi Tanzania imeichapa Namungo FC mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mabao ya Polisi Tanzania leo yamefungwa na Kassim Haruna dakika ya saba na Gerald Mathias dakika ya 19, wakati la Namungo limefungwa na Freddy Tangalo dakika ya 57.
Kwa ushindi huo, Polisi Tanzania inafikisha pointi 34 baada ya kucheza mechi 25 na kusogea nafasi ya saba, wakati Namungo inabaki na pointi zake 28 za mechi 20 sasa katika nafasi ya 12.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Ihefu SC imeichapa Mbeya City 1-0, bao pekee la Andrew Simchimba dakika ya 74 Uwanja wa Highland Estate, Ubaruku, Mbarali, Mbeya.
Ihefu SC inafikisha pointi 24 baada ya kucheza mechi 26 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 16, ikiizidi pointi tatu Mbeya City ambayo ina mechi moja mkononi.